Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeanzisha Kijiji cha Mazingira katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), kikilenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira.
Kijiji hicho kimekuwa jukwaa la kukutanisha wananchi, wadau wa mazingira na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuonesha ubunifu na teknolojia rafiki kwa mazingira pamoja na kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali za asili.
Katika kijiji hicho, wananchi wanapata elimu kuhusu usimamizi wa taka, urejelezaji wa bidhaa, uhifadhi wa bioanuwai na utekelezaji wa sheria za mazingira.
Wataalamu kutoka NEMC na taasisi mbalimbali pia wanatoa ushauri wa kitaalamu na kujibu maswali ya wananchi kuhusu changamoto za mazingira.
NEMC imesema ushiriki wake katika maonesho ya Sabasaba ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira ili kuhakikisha maendeleo endelevu na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wananchi wamehamasishwa kutembelea Kijiji cha Mazingira kilichopo katika viwanja vya Sabasaba ili kujifunza, kushuhudia ubunifu mbalimbali wa wadau wa mazingira na kupata huduma za ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya mazingira.