Serikali imezitaka taasisi za umma na binafsi nchini kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi huku ikisisitiza kuwa suala la faragha si jukumu la wataalamu wa TEHAMA pekee, bali ni sehemu ya uongozi, utawala bora na usimamizi wa hatari katika taasisi.
Wito huo umetolewa na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Fatma Zuberi Kalovya, wakati akifunga Kongamano la Kwanza la Taifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi 2026 lililofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.
Bi. Kalovya alisema Tanzania inaendelea kujenga uchumi wa kidijitali unaotegemea matumizi ya teknolojia, hivyo kulinda taarifa za wananchi ni jambo muhimu katika kujenga imani kwa watumiaji wa huduma za kidijitali.
"Hakuna uchumi wa kidijitali unaweza kusitawi bila imani, na hakuna matumizi salama ya teknolojia bila kuheshimu haki ya faragha ya mtu binafsi," alisema.
Alibainisha kuwa hadi Aprili 8, 2026, maelfu ya taasisi za umma na binafsi zilikuwa zimekamilisha usajili katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), hatua aliyoieleza kuwa ni ishara ya mwitikio mzuri wa wadau katika kutekeleza matakwa ya sheria.
Hata hivyo, alisema utekelezaji wa sheria hauishii kwenye usajili pekee, bali unahitaji taasisi kuweka mifumo, sera, taratibu na mafunzo ya kudumu ya kulinda taarifa binafsi.
Kwa niaba ya serikali, aliielekeza PDPC kuendelea kutoa elimu kwa umma, kufanya ukaguzi na kutoa mafunzo kwa maafisa wa ulinzi wa taarifa ili kuongeza uelewa wa sheria hiyo kwa wananchi wa mijini na vijijini.
Aidha, alisisitiza kuwa sekta binafsi inapaswa kuona ulinzi wa taarifa binafsi kama uwekezaji unaojenga imani kwa wateja na kuongeza ushindani, badala ya kuuchukulia kama gharama ya uendeshaji.
Bi. Kalovya pia alitoa wito wa kueneza kauli mbiu ya "Your Privacy" kwa lugha rahisi zaidi ili kila Mtanzania, wakiwemo wananchi wa vijijini, aweze kuelewa haki zake za faragha na namna ya kuzilinda.
Kongamano hilo liliwakutanisha viongozi wa taasisi, wataalamu wa TEHAMA, wadhibiti, sekta binafsi, wasomi na washirika wa maendeleo kutoka Tanzania na nchi mbalimbali, likilenga kujadili mustakabali wa faragha na ulinzi wa taarifa binafsi katika enzi ya uchumi wa kidijitali.