Na Atley Kuni, WAF – Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemwapisha Dkt. Grace Elias Magembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, akimpa jukumu la kusimamia utekelezaji wa sera, mipango na bajeti ya sekta hiyo muhimu ya afya nchini.
Hafla hiyo ya kuapishwa imefanyika Julai 1, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam na kurushwa mubashara na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Samia amesema uteuzi wa Dkt. Magembe umetokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika utumishi wa umma, akieleza kuwa ana imani na uwezo wake wa kuleta matokeo katika sekta ya afya.
Amesema Dkt. Magembe anakwenda kusimamia Wizara ya Afya katika kipindi ambacho Bunge limepitisha bajeti muhimu ya sekta hiyo, hivyo akamtaka kuhakikisha kila fedha inayotolewa inatumika kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.
“Unakwenda kusimamia bajeti ambayo imepitishwa na Bunge. Hakikisha utekelezaji wake unaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi na kila shilingi inatumika kwa uadilifu na kwa manufaa ya Watanzania,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amemtaka Katibu Mkuu huyo mpya kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unaimarika katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini, akisisitiza kuwa wananchi wanatarajia huduma bora na kwa wakati.
“Wananchi wanahitaji kuona dawa zinapatikana, vifaa tiba vinakuwepo na huduma zinatolewa kwa ubora unaostahili. Hilo ni jukumu ambalo lazima lisimamiwe kwa karibu,” amesema.
Katika maelekezo yake, Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa uongozi shirikishi ndani ya Wizara ya Afya, akimtaka Dkt Magembe kujenga mahusiano mazuri na watumishi wa umma.
“Nenda ukaishi vizuri na watumishi. Washirikishe, wasikilize na waongoze kwa haki, kwa sababu mafanikio ya wizara yanajengwa na timu, si mtu mmoja,” amesema.
Rais Samia ameongeza kuwa Serikali itaendelea kumpa ushirikiano Dkt Magembe katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.