| Picha hii imetengenezwa kwa msaada wa akili unde kwa malengo ya kuhabarisha pekee |
Na Charles Mkoka
Dar es Salaam. Tanzania Mercantile Exchange (TMX) imeendelea kuimarisha uwazi katika biashara ya mazao kwa kutumia Kitengo cha Market Desk, kinachokusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za bei za mazao, matokeo ya minada na taarifa rasmi za soko kwa wakati halisi.
Kupitia kitengo hicho, TMX hutoa taarifa za kila siku kuhusu bei za mazao baada ya minada ya kidijitali, huku pia ikiandaa ripoti za mwenendo wa soko zinazowasaidia wakulima, wanunuzi, vyama vya ushirika (AMCOS), madalali na wadau wengine kufanya maamuzi sahihi ya biashara.
Mbali na kuchapisha taarifa za bei, Market Desk husambaza takwimu kupitia vyombo vya habari na mifumo ya kidijitali ili kuhakikisha wakulima kote nchini wanapata taarifa sahihi kuhusu thamani ya mazao yao. Pia huendesha huduma maalumu ya mawasiliano inayowawezesha wadau kupata takwimu za biashara na mwenendo wa soko kwa haraka.
Kwa mujibu wa TMX, zaidi ya tani milioni mbili za mazao ya kilimo zimeuzwa kupitia mfumo huo tangu kuanzishwa kwake, huku thamani ya biashara ikizidi TShs. Trilioni 5.8. Mfumo huo umeendelea kuongeza uwazi wa biashara na kupunguza utegemezi wa madalali wasiokuwa rasmi.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mazao kama ufuta, korosho, kahawa, mbaazi na dengu yanaendelea kuuzwa kupitia minada ya kidijitali katika maeneo mbalimbali nchini, huku bei zikibadilika kulingana na ubora wa zao, eneo la ghala na ushindani wa wanunuzi.
TMX imeeleza kuwa taarifa zote za bei, ripoti za soko na matokeo ya minada hupatikana kupitia mifumo yake rasmi, hatua inayolenga kuwapa wadau taarifa za uhakika na kuongeza ufanisi wa biashara ya mazao nchini.