Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeanza rasmi maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), huku Serikali ikizitaka wizara, taasisi za umma, sekta binafsi, watafiti na mashirika ya kiraia kutumia mkutano huo kama jukwaa la kuonyesha ubunifu, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ajenda ya uchumi wa buluu.
Akizungumza jijini Tanga Julai 2, 2026 wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika Oktoba 6 hadi 9 mwaka huu, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee kuonyesha hatua ilizopiga katika usimamizi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani.
Kwa mujibu wa Kwagilwa, Tanzania ilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mkataba wa Nairobi kwa kipindi cha miaka miwili wakati wa mkutano wa COP11 uliofanyika Madagascar mwaka 2024, huku pia ikipewa heshima ya kuandaa COP12.
Mbali na kupokea mamia ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali, mkutano huo unatarajiwa kujadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mkataba wa Nairobi wa kipindi cha 2024 hadi 2026 pamoja na masuala yanayohusu uhifadhi na urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya bahari ikiwemo mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuipa uzito agenda ya mazingira kwa kutambua kuwa uchumi wa buluu ni miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo ya muda mrefu.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeiweka sekta hiyo kama eneo la kimkakati linalotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha ya wananchi na kulinda mazingira kwa wakati mmoja.
"Tanzania ni nchi ya pwani yenye fursa kubwa katika sekta za uvuvi, utalii, usafirishaji, nishati, madini na viwanda. COP12 ni nafasi ya kuonesha uwezo huo na kujenga ushirikiano utakaosaidia kufikia maendeleo endelevu," amesema.
Hata hivyo, wakati Serikali ikijipanga kutumia mkutano huo kufungua fursa mpya, Mkoa wa Tanga umeeleza kuwa tayari athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuonekana kwa kiwango kikubwa katika shughuli zinazotegemea bahari.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2021 na 2025 umeonyesha ongezeko la joto la bahari kutoka nyuzi joto 25.6 mwaka 2021 hadi kufikia nyuzi joto 28.39 mwaka 2024.
Kwa mujibu wake, mabadiliko hayo yameathiri mfumo wa ikolojia wa bahari na kusababisha changamoto katika sekta ya uvuvi pamoja na ukuzaji wa viumbe maji, hususan kilimo cha mwani.
"Tumeshuhudia ongezeko la karibu nyuzi joto tatu baharini, huku siku za wavuvi kwenda kuvua zikishuka kutoka siku 221 mwaka 2021 hadi siku 170 kutokana na upepo mkali na hatari ya usalama baharini. Pia mavuno ya samaki yamepungua kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30," amesema Burian.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda, amesema mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki kati ya 500 na 600 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo viongozi wa serikali, wataalamu na wadau wa mazingira.
Amesema tamko la Serikali limezindua rasmi maandalizi ya kitaifa kwa lengo la kuweka vipaumbele na kuhakikisha Tanzania inaingia kwenye mkutano huo ikiwa imejipanga kikamilifu.
Mkataba wa Nairobi, ambao Tanzania ni mwanachama wake, ulisainiwa Juni 21, 1985 na unasimamiwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). Unalenga kuhifadhi, kusimamia na kuendeleza mazingira ya bahari pamoja na ukanda wa pwani wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.