Dkt. Grace Magembe apewa jukumu la kusimamia mageuzi makubwa ya sekta ya afya

Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Elias Magembe, akiapishwa rasmi kushika wadhifa huo katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Picha na: Ikulu Mawasiliano

 Na Charles Mkoka

Dkt. Grace Elias Magembe ameibuka kuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika sekta ya afya nchini baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa Juni 2026.

Daktari huyo mwenye uzoefu wa miaka mingi katika tiba, afya ya umma na usimamizi wa sera za afya amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na baadaye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya katika Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kabla ya kuteuliwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali Januari 2025.

Katika utumishi wake, Dkt. Magembe amewahi kuwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tiba katika Wizara ya Afya, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya katika Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mganga Mkuu wa Serikali na sasa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.

Uteuzi wake kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ni hatua mpya katika safari yake ya utumishi wa umma na unakuja wakati Tanzania ikiendelea na jitihada za kufikia huduma za afya kwa wote, kuimarisha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ndani ya nchi pamoja na kuendeleza matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya.

Moja ya majukumu makubwa anayotarajiwa kusimamia ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia la kuhakikisha Tanzania inafikia angalau asilimia 60 ya kujitosheleza kwa dawa na vifaa tiba ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Grace Elias Magembe ameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya katika hafla ya kuapishwa viongozi iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, akianza jukumu jipya la kusimamia utendaji wa wizara hiyo. Picha: Ikulu Mawasiliano

Dkt. Magembe pia amekuwa sauti muhimu katika kuimarisha afya ya uzazi, mama na mtoto. Kabla ya kujiunga na uongozi wa juu serikalini, aliwahi kuwa Meneja wa Programu za Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Mchanga katika taasisi ya Amref Health Africa Tanzania.

Katika kipindi chake cha utumishi, amesifiwa kwa kusimamia mifumo ya kidijitali ya afya, kuhamasisha matumizi ya telemedicine na kuongoza hatua mbalimbali za kukabiliana na milipuko ya magonjwa, ikiwemo ugonjwa wa Marburg uliotokea kaskazini-magharibi mwa Tanzania, Magonjwa ya mafua ya UVIKO 19 na Kipindupindu, kilichoisumbua miaka ya nyuma jijini Dar es salaam.

Aidha, ameshiriki kwa miaka zaidi ya 20 katika kuanzisha na kuimarisha huduma za matibabu ya VVU nchini, huku akiongoza juhudi za kuboresha huduma za wagonjwa wa selimundu na hemofilia.

Dkt. Magembe ana Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma pamoja na Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara kutoka Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI).

Mbali na utumishi wake serikalini, amewahi kuhudumu katika bodi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, zikiwemo Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) na Tanzania Health Summit, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa viongozi wa afya wenye ushawishi mkubwa nchini na kanda ya Afrika Mashariki.