TMDA yapiga marufuku dawa za Levamisole kwa mifugo


Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetangaza kupiga marufuku matumizi ya dawa zote za mifugo zenye kiambata cha Levamisole nchini Tanzania, ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda afya ya binadamu, wanyama na usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMDA iliyotolewa Juni 24, 2026, tafiti na tathmini zimeonyesha kuwa mabaki ya dawa hiyo yanaweza kubaki kwenye nyama na maziwa ya wanyama waliotibiwa, hali inayoweza kuhatarisha afya ya walaji. 

Aidha, matumizi yasiyo sahihi ya Levamisole yanaweza kusababisha sumu kwa mifugo na madhara mbalimbali.

TMDA imeeleza kuwa kuanzia sasa dawa zote zenye kiambata hicho hazitaruhusiwa kutengenezwa, kuingizwa nchini, kusambazwa, kuuzwa wala kutumika. 

Mamlaka hiyo imefafanua kuwa marufuku hiyo inaanza kutekelezwa mara moja.

Wafugaji, wafanyabiashara na wasambazaji wote wa dawa hizo wametakiwa kusitisha shughuli zote zinazohusiana na Levamisole na kuzirudisha katika ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza, Geita, Morogoro, Tabora, Ruvuma na Kagera kabla ya Julai 14, 2026.

TMDA imewahimiza wafugaji kutumia dawa za mifugo zilizosajiliwa na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ya mifugo ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula salama kwa walaji. 

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa zote zinazopatikana sokoni.