DCEA yakamata Tani 22.6 za Dawa za Kulevya ndani ya miezi miwili, watuhumiwa 188 wanaswa


Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 22.6 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika nchini kati ya Mei na Juni 2026, huku watuhumiwa 188 wakikamatwa na mali mbalimbali zinazohusishwa na biashara hiyo zikitaifishwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya DCEA iliyotolewa Alhamisi Julai 2, operesheni hizo pia zilinasa lita 30.5 za bidhaa zenye kemikali ya THC, kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, na kuteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi pamoja na tani 3.3 za bangi na mirungi. 

Aidha, magari sita, bajaji mbili na pikipiki 33 zilikamatwa zikihusishwa na mtandao wa biashara hiyo haramu.

Katika moja ya matukio makubwa, DCEA ilikamata bidhaa zilizoandikwa kuwa ni virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Uchunguzi wa maabara ulibaini kuwa bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha Prazepam, dawa yenye asili ya kulevya inayoweza kusababisha uraibu, kuathiri mfumo wa fahamu na hata kusababisha kifo endapo itatumika bila usimamizi wa daktari. 

Bidhaa hizo zilikuwa zimeingizwa kutoka Malaysia na zilitarajiwa kusafirishwa kwenda Barbados, huku watu watatu wakikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Katika operesheni nyingine jijini Dar es Salaam, mamlaka ilikamata lita 30.5 za vinywaji vya kuongeza nguvu vya chapa ya TRIP baada ya kubainika kuwa vilikuwa na kemikali ya THC, ambayo ndiyo kiambata kikuu kinachopatikana kwenye bangi. Vinywaji hivyo vilikutwa katika duka la Village Supermarket, na watu wawili walikamatwa kwa ajili ya hatua za kisheria.

Mbali na Dar es Salaam, ukamataji mkubwa ulifanyika katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na maeneo mengine ya nchi, ambapo tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 40 za skanka na kiasi cha heroin vilinaswa. 

Mashamba ya bangi yaliyokuwa Dodoma, Lindi, Geita na Sengerema pia yaliteketezwa katika operesheni hizo.

DCEA imesema imeongeza ushirikiano na mamlaka za Eswatini, Afrika Kusini, Msumbiji na Zambia kufuatilia Watanzania wanaodaiwa kuhusika na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya waliokimbilia katika nchi hizo. 

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa operesheni za pamoja zitaendelea sambamba na ukaguzi wa bidhaa, dawa na virutubisho ili kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia mpya.