Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetangaza uzinduzi wa programu ya mafunzo na vyeti kwa Maafisa Ulinzi wa Taarifa (DPOs), hatua inayolenga kuongeza weledi katika usimamizi wa faragha na usalama wa taarifa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, alisema programu hiyo ya Certified Data Protection Authorized (CDPA) itazinduliwa rasmi Julai 13, 2026 kwa ushirikiano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Kwanza la Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dkt. Mkilia alisema mafunzo hayo yatatolewa kwa njia ya mtandao na ana kwa ana ili kuwafikia wataalamu wengi zaidi nchini.
“Tunataka kuwa na Maafisa Ulinzi wa Taarifa wenye ujuzi wa kutosha ili kusaidia taasisi kutekeleza sheria kwa ufanisi na kupunguza vihatarishi vya faragha,” alisema.
Alisema kongamano hilo la siku tatu limeweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi, huku Tanzania, Kenya na Uganda zikikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za faragha zinazochangiwa na ukuaji wa teknolojia.
Dkt. Mkilia alisema changamoto za ulinzi wa taarifa zinafanana katika nchi za Afrika Mashariki, hivyo kuna umuhimu wa kushirikiana ili kujenga uchumi wa kidijitali ulio salama na unaoaminika.
Aidha, PDPC ilisema itaendelea kutumia mbinu jumuishi inayoshirikisha sekta ya umma, sekta binafsi na wataalamu wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Kongamano hilo, ambalo ni la kwanza kufanyika nchini, linatarajiwa kuwa la kila mwaka na ni sehemu ya jitihada za Tanzania kujiandaa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuimarisha uchumi wa kidijitali.