Na Mwandishi Wetu, Mtwara
Wakazi wa Kijiji cha Mbangala Mbuyuni na maeneo jirani wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara, wameondokana na changamoto ya muda mrefu ya usafiri na upatikanaji wa huduma za kijamii kufuatia kukamilika kwa daraja la mawe lililojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Daraja hilo limejengwa kupitia Mradi wa RISE chini ya programu ya kuondoa vikwazo vya barabara (Bottleneck), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Nanyumbu, Mhandisi Dikson Mkokota, alisema zaidi ya Shilingi milioni 195 zimetumika kujenga boksi kalavati la mawe katika barabara ya Nanyumbu-Mbangala Mbuyuni ili kuondoa tatizo la maji yaliyokuwa yakikatisha mawasiliano kati ya vijiji hivyo.
“Hili lilikuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi kufika Nanyumbu kupata huduma za afya, elimu na kufanya shughuli za biashara. Sasa mawasiliano yameimarika kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa daraja hilo pia litarahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kwenda katika maghala ya Nanyumbu na Mangaka, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wakulima wa eneo hilo.
Mkazi wa Mbangala Mbuyuni, Marijani Mohamed, alisema kabla ya mradi huo wananchi walilazimika kuzunguka kupitia vijiji vya jirani ili kufika Nanyumbu, jambo lililoongeza gharama na kupoteza muda.
“Tulikuwa tunateseka sana, hasa wakati wa mvua. Sasa tunafika Nanyumbu kwa urahisi na gharama zimepungua,” alisema.
Kupitia Mradi wa RISE, TARURA inaendelea kutekeleza miradi ya kuondoa vikwazo vya barabara katika maeneo mbalimbali ya vijijini kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.