Na Charles Mkoka, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya kiasi cha rekodi cha TShs37.957 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26, ikivuka lengo la TShs. 36.66 trilioni na kufikia ufanisi wa asilimia 105.24.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema mafanikio hayo yanaonesha ukuaji wa asilimia 17.6 ikilinganishwa na Sh32.27 trilioni zilizokusanywa mwaka uliopita.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na uzinduzi wa Tuzo ya Rais kwa Walipakodi yaliyofanyika Julai 1 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Mwenda alisema TRA imeandika historia mpya kwa kufikia au kuvuka malengo ya makusanyo kwa miezi 24 mfululizo.
“Mwezi Juni pekee tumekusanya mapato ghafi ya TShs.trilioni 4.014 . Hii ni rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu TRA ilipoanzishwa miaka 30 iliyopita,” alisema.
Mwenda alisema idadi ya walipakodi nchini imeongezeka kutoka walipakodi 75 elfu mwaka 1996 hadi zaidi ya milioni 8.1 mwaka 2026, hatua inayodhihirisha kupanuka kwa uchumi na kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika ulipaji wa kodi.
Alisema TRA imepitia mageuzi makubwa ya kiteknolojia, ikihama kutoka mifumo ya karatasi kwenda mifumo ya kidijitali, matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD), stempu za kielektroniki na malipo ya kidijitali.
Kamishna Mkuu huyo alisema mamlaka hiyo imejipanga kuunga mkono azma ya Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja kupitia upanuzi wa wigo wa walipakodi, kuboresha mifumo ya kodi, kudhibiti magendo na kuimarisha usimamizi wa kodi za kimataifa.
Aidha, alitangaza kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mamlaka za Kodi za Jumuiya ya Madola (CATA) utakaofanyika Septemba 5, 2026 mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wa mamlaka za kodi kutoka nchi 48 wanachama.
Mwenda alisema kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni ishara ya kuongezeka kwa hadhi ya nchi kimataifa na matokeo ya sera za kiuchumi zinazoendelea kutekelezwa.