Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Tuzo ya Rais kwa Walipakodi Bora kwa mara ya kwanza nchini, akisema walipakodi waaminifu wanastahili kutambuliwa kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rais Samia alisema ukusanyaji wa mapato ya ndani ni msingi wa kujitegemea kiuchumi na kufanikisha agenda ya maendeleo.
“Tunatuma ujumbe kwamba serikali inatambua, inathamini na inaheshimu mchango wa walipakodi katika ujenzi wa taifa,” alisema.
Rais Samia alisema serikali imekamilisha mapitio ya mfumo wa kodi yaliyolenga kuifanya Tanzania kuwa na mfumo wa kodi ulio rahisi, wa haki na unaochochea ulipaji wa hiari.
Aidha, aliwataka watumishi wa TRA kutumia teknolojia, weledi na uadilifu katika ukusanyaji wa mapato badala ya kutumia mabavu au kuwanyanyasa wafanyabiashara.
“Tusitumie nguvu wala kuwaonea wafanyabiashara. Tutumie maarifa, teknolojia na weledi katika ukusanyaji wa mapato,” alisema.
Rais Samia pia alisisitiza kuwa kulipa kodi si wajibu wa kisheria pekee, bali ni kitendo cha uzalendo na heshima kwa taifa.
“Ukwepaji kodi ni usaliti na haupaswi kuwa jambo la kujivunia,” alisema.
TRA ilianzishwa mwaka 1995 na imeendelea kuwa taasisi muhimu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii nchini.