Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Kupitia banda lake, REA inatoa taarifa kuhusu miradi ya umeme vijijini na pembezoni mwa miji pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
Wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kufahamu maendeleo ya miradi ya kusambaza umeme, maeneo yanayonufaika na miradi mipya pamoja na mipango ya serikali ya kuendelea kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.
Aidha, REA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama kwa afya na mazingira.
Pia, REA imewataka wadau, wananchi na wawekezaji kutembelea banda lake ili kupata maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi ya nishati na fursa zilizopo katika sekta hiyo.
Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yalianza Juni 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania."
