Uamuzi wa Serikali kuikabidhi Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ujenzi wa barabara za kuingia katika uwanja wa michezo wa AFCON jijini Arusha umetajwa kuwa ishara ya imani kubwa kwa uwezo wa wataalamu na taasisi za ndani katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Tanzania, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, inajiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kupitia mradi huo, TARURA itasimamia ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara inayotarajiwa kurahisisha usafiri wa wachezaji, viongozi, mashabiki na watalii watakaofika Arusha wakati wa mashindano hayo.
Katika miaka ya karibuni, TARURA imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara nchini, hatua iliyochangia kuimarika kwa usafirishaji, biashara, utalii na utoaji wa huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa Serikali, mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa Design and Build, ambapo mkandarasi mmoja anawajibika kuandaa usanifu na kutekeleza ujenzi wa barabara hizo.
Mfumo huo unalenga kuharakisha utekelezaji wa mradi, kupunguza ucheleweshaji wa kiutawala na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa kazi.
Mbali na maandalizi ya AFCON, barabara hizo zinatarajiwa kuendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa Arusha kwa kuboresha usafiri, kuimarisha utalii na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma hata baada ya mashindano kumalizika.
Wachambuzi wa miundombinu wanaona mradi huo kama fursa kwa TARURA kuonesha uwezo wake wa kusimamia miradi mikubwa yenye viwango vya kimataifa na kuendelea kujijengea nafasi kama moja ya taasisi muhimu katika maendeleo ya miundombinu nchini.