PBPA: SCADA yapunguza upotevu wa mafuta wakati wa ushushaji

 

Na Mwandishi wetu

Dodoma. Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa uingizaji wa mafuta nchini kupitia matumizi ya mfumo wa kidijitali wa Supervisory Control and Data Acquisition (SCADA) unaowezesha kufuatilia mafuta kwa wakati halisi kuanzia yanaposhushwa kutoka melini hadi yanapohifadhiwa maghalani.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mhandisi wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Elvira Muganga, amesema mfumo huo umeongeza uwazi na ufanisi katika kudhibiti upotevu wa mafuta wakati wa shughuli za ushushaji.

Amesema SCADA hukusanya taarifa kutoka kwenye mita za Serikali zilizowekwa katika maeneo ya kupokelea mafuta na kuzilinganisha na taarifa kutoka kwenye mita za maghala ya kuhifadhia mafuta.

"Lengo ni kuhakikisha kiwango cha mafuta kinachoshushwa kutoka melini kinafanana na kile kinachopokelewa maghalani, hivyo kubaini mapema tofauti zozote zinazoweza kujitokeza," amesema.

Muganga amesema kabla ya matumizi ya mfumo huo, ufuatiliaji wa ushushaji wa mafuta ulitegemea zaidi taarifa za kawaida, hali iliyofanya uthibitishaji wa taarifa kwa wakati kuwa mgumu.

Ameeleza kuwa matumizi ya SCADA yameongeza uwazi, uwajibikaji na usahihi wa taarifa zinazotumika kusimamia uingizaji wa mafuta pamoja na kukokotoa mapato ya Serikali.

Kwa mujibu wa PBPA, mfumo huo pia umeiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazotumia teknolojia za kisasa kusimamia shughuli za uingizaji wa mafuta na kupunguza upotevu unaoweza kujitokeza wakati wa kuhamisha mafuta kutoka melini kwenda kwenye maghala.

Katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu, PBPA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo wa SCADA, Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS) na nafasi ya wakala huo katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini unakuwa wa uhakika, salama na wenye uwazi.

Muganga amewaalika wananchi na wadau wa sekta ya nishati kutembelea banda la PBPA ili kujifunza zaidi kuhusu mifumo ya kisasa inayotumika kusimamia sekta ya mafuta nchini.