Dar es Salaam kuwa kitovu cha maonesho makubwa ya kilimo Afrika

 
Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa maonesho makubwa ya kilimo, mifugo na usindikaji wa chakula barani Afrika, yatakayofanyika Septemba 2 hadi 3, 2026 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Maonesho hayo ya 10th Africa Agri Expo (AAE 2026) yatafanyika sambamba na Future Food, Livestock and Poultry Expo (FLIP 2026), yakitarajiwa kukutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 35 kujadili fursa za biashara, teknolojia na uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Waandaaji wamesema zaidi ya wageni 10,000 wanatarajiwa kuhudhuria maonesho hayo, huku kampuni zaidi ya 1,000 kutoka sekta za kilimo, mifugo, chakula na usindikaji zikishiriki kupitia waoneshaji na washirika mbalimbali.

Aidha, waoneshaji zaidi ya 125, wadhamini pamoja na wataalamu 75 watawasilisha teknolojia na ubunifu mpya katika kilimo, ikiwemo mitambo ya kisasa, umwagiliaji, mbegu bora, vifaa vya ufugaji, lishe ya mifugo na teknolojia za usindikaji wa chakula.

Mbali na maonesho, kutakuwa na kongamano litakalowakutanisha zaidi ya washiriki 750 kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa kujadili mwelekeo wa sekta ya kilimo na mifugo barani Afrika.

Waandaaji wamesema maonesho hayo yatatoa fursa kwa wakulima, wasambazaji, wafanyabiashara na wawekezaji kukutana ana kwa ana na wazalishaji wa kimataifa, kujenga ushirikiano wa kibiashara, kupata uwakilishi wa bidhaa na kujifunza teknolojia mpya zinazoweza kuongeza tija.

Pia, taasisi na vyama mbalimbali vya kilimo na mifugo kutoka Afrika Mashariki vitashiriki, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika biashara, uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.

Kwa mujibu wa waandaaji, Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake muhimu katika uchumi wa kilimo Afrika Mashariki na uwekezaji unaoendelea katika kuongeza thamani ya mazao, mifugo na uzalishaji wa chakula.

Wadau wa kilimo, mifugo, usindikaji wa chakula, wawekezaji, washauri wa biashara na taasisi za umma wamehimizwa kushiriki maonesho hayo ambayo yanatajwa kuwa miongoni mwa makubwa zaidi ya biashara ya kilimo barani Afrika mwaka huu.