Na Charles Mkoka
Lindi – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka amesema sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zinapaswa kuhamia katika uzalishaji unaolenga soko na kuongeza thamani ya mazao ili kuchochea uchumi shindani unaokusudiwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri Nanauka alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua rasmi Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mhe. Nanauka alisema maonesho ya Nanenane ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa yanafanyika baada ya kuanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 Julai 1, mwaka huu. Dira hiyo inalenga kujenga uchumi jumuishi, wenye ushindani na unaotegemea uzalishaji wenye tija na thamani kubwa.
Amesisitiza kuwa Kaulimbiu ya Nanenane 2026, "Tambua soko, ongeza tija kuelekea Dira ya Taifa 2050," inapaswa kuwa mwongozo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko badala ya kuongeza uzalishaji pekee.
"Kufanikiwa kwa sekta hizi hakutategemea kuongeza uzalishaji tu, bali kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko, kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza thamani ili ziwe na ushindani ndani na nje ya nchi," alisema.
Pamoja na Tanzania kufanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya biashara, bado ipo changamoto kubwa ya kuyauza mazao mengi yakiwa ghafi.
Alitolea mfano wa zao la biashara la korosho, akisema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya korosho zinazozalishwa Lindi na Mtwara bado husafirishwa bila kuchakatwa.
Kwa mujibu wa Mhe. Nanauka, hali hiyo inawanyima wakulima na taifa faida kubwa zinazoweza kupatikana kupitia uchakataji wa mazao. Alihimiza uwekezaji zaidi katika viwanda vya kuongeza thamani na kuboresha ubora wa bidhaa ili ziweze kushindana katika soko la kimataifa.
Waziri huyo pia alisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwemo mahindi, mpunga, muhogo, mtama na mikunde, hatua inayoimarisha usalama wa chakula katika Kanda ya Kusini na kupunguza utegemezi wa mazao kutoka maeneo mengine ya nchi.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia miradi ya kimkakati pamoja na ruzuku ya pembejeo kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji.


