Na Mwandishi wetu
Lindi. Wakulima na wakazi wa mijini wamehimizwa kutumia mfumo wa kilimo cha mboga kwenye viroba ili kuongeza uzalishaji wa chakula hata katika maeneo yenye nafasi ndogo.
Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mtama, Yahya Salomo Nampapata, wakati akitoa elimu kwa wananchi kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Amesema mfumo huo unafaa zaidi kwa mazao ya mboga kama Chinese na spinach, huku ukiwawezesha hata watu wanaoishi mijini kuzalisha mboga kwenye maeneo madogo ya nyumbani.
"Nafasi ndogo siyo kikwazo cha kulima. Hata eneo la mita tano kwa tano linaweza kubeba viroba kadhaa na kukupa mboga za kutosha kwa matumizi ya familia," amesema.
Nampapata amesema hatua muhimu ni kuandaa kiroba chenye matundu ya kupitisha maji, kujaza mchanganyiko wa udongo, samadi iliyooza vizuri na mchanga, kisha kupanda mbegu au kuhamishia miche kutoka kwenye kitalu.
Amesisitiza matumizi ya samadi iliyooza vizuri, akieleza kuwa samadi mbichi, hususan ya kuku, inaweza kuharibu mimea kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha joto.
"Samadi ya kuku inafaa, lakini lazima iwe imekauka na kuoza vizuri. Ikiwa mbichi inaweza kuunguza mimea," amesema.
Ameongeza kuwa mazao hayo yanahitaji kumwagiliwa maji asubuhi na jioni hadi yatakapokomaa, huku mfumo huo ukiwa rahisi kutekelezwa na mtu yeyote bila kuhitaji eneo kubwa.
Kwa wakulima wanaohitaji kuanzishiwa bustani za viroba majumbani, amesema maafisa kilimo wako tayari kutoa ushauri wa kitaalamu na kusaidia kuandaa mfumo huo ili wananchi wengi zaidi wanufaike na kilimo cha mboga za majumbani.

