Tanzania yaandika historia kwa kuuza bondi ya kwanza ya shilingi London

Picha hii imetengenezwa kwa msaada wa akili Unde (AI)

 Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Tanzania imeandika historia katika masoko ya fedha duniani baada ya bondi yake ya kwanza ya shilingi ya Tanzania kuorodheshwa katika Soko la Hisa la London (London Stock Exchange), hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa biashara ndogo na za kati nchini.

Bondi hiyo yenye thamani ya Sh262.5 bilioni (sawa na dola za Marekani milioni 100) imetolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), ambalo ni taasisi ya Benki ya Dunia inayosaidia sekta binafsi, huku fedha hizo zikielekezwa kupitia Benki ya NMB kwa ajili ya kuongeza mikopo kwa biashara ndogo, za kati na zinazokua (MSMEs).

Takribani asilimia 20 ya fedha hizo zimetengwa mahsusi kusaidia biashara zinazomilikiwa na wanawake, ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema kuwa hatua hiyo inaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa kwa uchumi wa Tanzania na inaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia upatikanaji wa vyanzo vipya vya fedha.

Kwa mujibu wa IFC, bondi hiyo ni ya kwanza ya aina yake kutolewa kwa shilingi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa na pia ndiyo kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa sarafu hiyo nje ya nchi. Ina riba ya asilimia 7.60 inayolipwa mara mbili kwa mwaka na itakomaa kuanzia Juni 15, 2031.

Tofauti na mikopo inayokopwa kwa fedha za kigeni, mfumo huu unaiwezesha Tanzania kuvutia mitaji kutoka kwa wawekezaji wa kimataifa bila kuongeza moja kwa moja hatari ya mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni.

Serikali inatarajia fedha hizo kusaidia kuongeza mikopo kwa sekta binafsi, kuchochea uwekezaji na kuzalisha ajira kati ya 13,000 na 20,000 kupitia ukuaji wa biashara zinazopata ufadhili.

Hatua hiyo pia inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazozidi kutumia masoko ya kimataifa ya mitaji kupata fedha za maendeleo, huku ikiimarisha nafasi yake mbele ya wawekezaji wa kimataifa.