Medinova yazindua idara ya tibamazoezi, yaongeza huduma za kibingwa

 

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Hospitali ya Medinova Specialized Polyclinic imezindua rasmi Idara ya Tibamazoezi (Physiotherapy) ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupanua huduma za afya za kibingwa na kuongeza upatikanaji wa huduma za ukarabati kwa Watanzania.

Hospitali hiyo inayomilikiwa na kampuni ya 33 Holding kutoka Qatar, imesema huduma hiyo itasaidia wagonjwa wanaopata nafuu baada ya upasuaji, ajali, kiharusi na magonjwa mengine yanayoathiri uwezo wa kutembea au kufanya shughuli za kila siku.

Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali hiyo, Dkt. Imran Asif Bwaja, amesema Medinova inaendelea kupanua huduma zake tangu ilipoanzishwa takribani miaka mitatu iliyopita, huku mipango ikiwa ni kuongeza vyumba vya upasuaji, huduma za dharura na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Amesema mazingira mazuri ya uwekezaji nchini yameiwezesha sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika huduma za afya, akiwapongeza viongozi wa Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Dkt. Selestine Mpiri, amesema tibamazoezi ni huduma ya kitaalamu inayotumia mazoezi maalumu, mbinu za mikono na vifaa tiba kurejesha uwezo wa mwili bila kutumia dawa au upasuaji.

Alisema watu wengi bado huchanganya tibamazoezi na masaji, wakati ukweli ni kwamba tibamazoezi hulenga kubaini chanzo cha tatoizo na kutoa tiba ya muda mrefu badala ya kupunguza maumivu kwa muda mfupi.

"Tibamazoezi si kwa wagonjwa wa ajali pekee. Huduma hii pia huwasaidia wenye maumivu ya mgongo, shingo, magoti, waliopata kiharusi, matatizo ya mfumo wa fahamu, magonjwa ya kupumua na changamoto nyingine nyingi," amesema.

Dkt. Mpiri pia amewatahadharisha wananchi dhidi ya kufuata mazoezi ya tiba yanayopatikana kwenye mitandao ya kijamii bila ushauri wa mtaalamu, akisema kila mgonjwa anatakiwa kupimwa na kupewa mpango wa tiba unaoendana na hali yake.

Kwa upande wake, mtaalamu wa tibamazoezi wa Medinova, Witney Lema, amesema idara hiyo inalenga kuwasaidia wagonjwa kurejesha uwezo wa kufanya shughuli zao za kila siku, kuongeza uimara wa mwili na kuboresha ubora wa maisha kupitia programu maalumu za ukarabati.

Mbali na tibamazoezi, Medinova inaendelea kutoa huduma nyingine za kibingwa zikiwemo magonjwa ya ndani, watoto, afya ya wanawake, ngozi, meno, tiba za urembo pamoja na huduma za maabara, huku ikipanga kuendelea kupanua huduma zake ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi kwa gharama nafupu.