Mkutano wa UNESCO wahitimishwa Busan, Tanzania yaahidi kuendeleza uhifadhi wa urithi

 Na Mwandishi wetu

Busan, Korea Kusini. Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia wa UNESCO umehitimishwa rasmi jijini Busan, Korea Kusini, baada ya siku kadhaa za mijadala kuhusu uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya maeneo ya urithi wa dunia.

Mkutano huo uliwakutanisha nchi wanachama wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 pamoja na wadau wa kimataifa kujadili hali ya uhifadhi wa maeneo yaliyopo kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia, kupitia maombi ya maeneo mapya na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoathiri urithi wa asili na wa kiutamaduni.

Tanzania ilishiriki mkutano huo chini ya ujumbe ulioongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Balozi Saidi Yakubu, aliyewasilisha msimamo wa nchi katika mijadala mbalimbali kuhusu uhifadhi wa urithi wa dunia, bioanuwai, usimamizi wa mifumo ya ikolojia na matumizi ya mbinu za kisayansi katika kuhifadhi mazingira.

Ujumbe wa Tanzania pia ulihusisha Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi.

Kwa mujibu wa NEMC, ushiriki wa Tanzania unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kutekeleza Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, kuimarisha usimamizi wa maeneo ya urithi wa dunia nchini na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi wa urithi wa asili na wa kiutamaduni.

Mkutano huo pia ulitoa fursa kwa Tanzania kubadilishana uzoefu na nchi nyingine, kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa kama UNESCO na IUCN, pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano wa kiufundi na kifedha kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi wa maeneo ya urithi wa dunia.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye maeneo yaliyotambuliwa na UNESCO kuwa Urithi wa Dunia kutokana na thamani yake ya kipekee, huku ushiriki wake katika mkutano huo ukiendelea kuimarisha nafasi ya nchi katika diplomasia ya mazingira na utekelezaji wa ajenda za maendeleo endelevu.