Na Mwandishi wetu
Busan, Korea Kusini. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kinachofanyika jijini Busan, Jamhuri ya Korea, kujadili masuala ya uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia na maendeleo endelevu.
Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Balozi Saidi Yakubu, ambaye anaiwakilisha nchi katika mijadala na maamuzi mbalimbali kuhusu uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia, bioanuwai, mifumo ya ikolojia na matumizi ya mbinu bora za usimamizi wa urithi wa asili na wa kiutamaduni.
Kikao hicho kimewakutanisha mataifa wanachama wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 pamoja na wadau mbalimbali wa kimataifa kupitia masuala ya uhifadhi na usimamizi wa maeneo yenye thamani ya kipekee duniani.
Miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa ni tathmini ya hali ya maeneo yaliyopo kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia, mapendekezo ya maeneo mapya ya kuorodheshwa pamoja na changamoto zinazoathiri urithi wa asili na wa kiutamaduni, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la shughuli za kibinadamu.
Kwa mujibu wa NEMC, ushiriki wa Tanzania unaonyesha dhamira ya Serikali kuendelea kutekeleza Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 na kuimarisha usimamizi wa maeneo ya urithi yaliyopo nchini.
Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Balozi Saidi Yakubu, na unawahusisha pia Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji.
Mbali na kushiriki mijadala, mkutano huo unaipa Tanzania fursa ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa kama UNESCO na IUCN, kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za uhifadhi na kutafuta fursa za ushirikiano wa kiufundi na kifedha.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyosaini Mkataba wa Urithi wa Dunia na inamiliki maeneo kadhaa yaliyotambuliwa na UNESCO kutokana na thamani yake ya kipekee ya kimataifa. Ushiriki wa NEMC katika kikao hicho unaendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira, bioanuwai na urithi wa dunia.

