HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI NA MEGA WE CARE WAANDAA KAMBI YA KUPIMA HOMA YA INI KUELEKEA JULAI 28


Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Mega We Care, imeanza maandalizi ya kambi maalumu ya uchunguzi wa homa ya ini kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani yatakayofanyika Julai 28.

Kambi hiyo itafanyika katika Kliniki ya Muhimbili Sokoine Drive Medical Centre (MNH-SDMC), iliyopo mkabala na Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dar es Salaam.

Lengo la kambi hiyo ni kuwapa wananchi fursa ya kupima homa ya ini mapema, kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuhamasisha wananchi kupata matibabu kwa wakati.

Katika maandalizi hayo, Mega We Care imetoa msaada wa dawa na vifaa tiba vitakavyotumika kutoa huduma kwa wananchi watakaofika kwenye kambi hiyo.


Afisa Habari wa Mega We Care, Mengi Ntasimba, alisema ushiriki wa kampuni hiyo ni sehemu ya kuwajibika kwa jamii kwa kushirikiana na wadau wa afya kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu.

"Tumeshiriki katika kampeni hii kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, hususan katika uchunguzi na uelewa wa homa ya ini," alisema.

Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani hufanyika kila Julai 28 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, kuhimiza uchunguzi wa mapema, kinga na matibabu ili kupunguza maambukizi na vifo vinavyotokana na homa ya ini.

Muhimbili imewahimiza wananchi kutumia fursa ya kambi hiyo kujua hali zao za afya na kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu kinga na matibabu ya homa ya ini.