Na Mwandishi wetu
Namtumbo, Ruvuma. Kamati ya Ukaguzi ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeutaka mkandarasi anayejenga Daraja la Muungano kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi huo ukamilike kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua.
Maelekezo hayo yalitolewa wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA, Henry Kaywanga, alisema mvua kubwa zinazonyesha eneo hilo husababisha shughuli za ujenzi kusimama, hivyo mkandarasi anapaswa kutumia kipindi kilichobaki kukamilisha kazi kwa wakati.
"Mkandarasi afunge taa eneo la mradi ili kazi ziendelee mchana na usiku. Pia aongeze wafanyakazi na vifaa vya ujenzi ili daraja likamilike kama ilivyopangwa," alisema.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Namtumbo, Mhandisi Fabian Lugalaba, alisema Daraja la Muungano ni mradi wa kimkakati unaolenga kumaliza changamoto ya kukatika kwa mawasiliano kati ya vijiji vya Minazini na Muungano, hasa kipindi cha masika.
Alisema wanafunzi wa Shule ya Msingi Ukombozi, wafanyabiashara na wananchi wamekuwa wakipata adha kubwa ya usafiri kutokana na mafuriko, hali inayotarajiwa kumalizika mara baada ya daraja hilo kukamilika.
"Daraja hili la zege lenye urefu wa mita 30 litahakikisha usafiri na usafirishaji vinaendelea mwaka mzima na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi," alisema.
Lugalaba pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kugharamia miradi ya miundombinu inayoboresha maisha ya wananchi na kuondoa changamoto za usafiri katika Wilaya ya Namtumbo.
Mkazi wa eneo hilo, Said Athumani, alisema daraja hilo litafungua fursa mpya za biashara, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuondoa tatizo la kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.
Kamati ya Ukaguzi ya TARURA ilihitimisha ziara yake mkoani Ruvuma baada ya pia kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mtyangimbole–Mnadani katika Wilaya ya Songea.