Dar es Salaam. Wanaume nchini wamehimizwa kujenga familia zinazodumu kwa kumweka Mungu mbele, kuimarisha mawasiliano na kushirikiana na wenza wao katika kila hatua ya maisha.
Wito huo ulitolewa katika semina ya uongozi iliyoandaliwa na Empower Leaders Ministry, chini ya Dominion Leadership and Research Institute (DLRI), iliyowakutanisha wababa, waume na vijana kujadili uongozi wa familia na maendeleo binafsi.
Semina hiyo ilisimamiwa na mtaalamu wa uongozi, Dkt. Sebastian Marondo, ambaye aliongoza mijadala mbalimbali kuhusu namna ya kujenga ndoa imara, malezi bora na uongozi unaozingatia misingi ya kiimani.
Kupitia mijadala na shuhuda za washiriki, semina ilijadili mambo mbalimbali ikiwemo changamoto zinazozikabili familia za sasa na umuhimu wa wanaume kujifunza stadi za uongozi, mawasiliano na malezi ili kuimarisha familia na jamii.
Mshiriki mmoja wa semina hiyo, Nathaniel Mjema, alisema amekuwa kwenye mahusiano kwa takribani miaka 50, yakiwemo maisha ya ndoa, lakini bado alipata mafunzo mapya yaliyomfanya kutafakari namna alivyoendesha maisha ya familia kwa miaka yote.
"Niligundua kuwa yapo mambo ambayo nimekuwa nikiyafanya kwa miaka mingi katika mahusiano na baadaye kwenye ndoa, lakini sikuwa na uelewa wa kutosha kama nilivyoupata leo," alisema.
Mjema alisema kama angepata mafunzo hayo mapema, angejenga msingi imara zaidi wa maisha ya familia.
"Mafunzo haya ningeyapata kabla, nahisi uelewa wangu ungekuwa imara zaidi. Nawasihi vijana na watu wa rika zote, bila kujali imani zao, kutafuta mafunzo haya. Kwa sasa dunia imebadilika, changamoto ni nyingi na mazingira yanatuweka wanaume katika maeneo ambayo wakati mwingine hata hatukutarajia kuwapo," alisema.
Aliongeza kuwa moja ya mafunzo makubwa aliyobeba ni umuhimu wa kumweka Mungu mbele katika kila jambo.
"Jambo liwe kubwa au dogo, anza na Mungu. Huo ndio msingi wa mafanikio," alisema.
Mjema pia alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya mume na mke pamoja na mawasiliano ya wazi ni nguzo muhimu za kujenga ndoa yenye afya na familia imara.
Naye mshiriki mwingine, Zabron Paul Makundi, ambaye amesema amekuwa kwenye ndoa kwa miaka 19 na ni mzazi wa watoto wanne, alisema uzoefu wake unaonyesha kuwa ndoa ni zaidi ya kuishi pamoja, bali ni agano linalohitaji uaminifu na kujitoa.
"Ndoa ni makubaliano ya watu wawili walioamua kuishi pamoja kwa maisha yanayompendeza Mungu. Lakini jambo kubwa zaidi linaloifanya idumu ni uaminifu," alisema.
Aliongeza kuwa wanandoa wanapaswa kujenga mahusiano yanayotawaliwa na kuaminiana, kuheshimiana na kushirikiana katika kutimiza majukumu ya familia.
Kwa mujibu wa waandaaji, semina hiyo ni sehemu ya juhudi za Empower Leaders Ministry za kuwajengea wanaume uwezo wa kuongoza familia, kukuza mahusiano bora na kuchangia ujenzi wa jamii yenye maadili.
Akihitimisha mijadala hiyo, Dkt. Sebastian Marondo aliwataka washiriki kuendelea kuwekeza katika ukuaji binafsi, kujifunza stadi za uongozi wa familia na kuzijengea familia zao misingi imara ya mawasiliano, uaminifu na maadili, akisisitiza kuwa familia imara ndiyo msingi wa jamii imara.