Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya malipo ya kidijitali, KuwaPay, imejiunga na mradi wa filamu ya Guardians of the Peak kama mdhamini rasmi wa msimu wa pili wa filamu hiyo, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya ubunifu na huduma za kifedha za kidijitali.
Ushirikiano huo unazikutanisha taasisi mbili zinazojikita katika ubunifu, maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimataifa. Wakati Guardians of the Peak ikiendelea kutumia filamu kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, nishati safi na utalii endelevu, KuwaPay inalenga kurahisisha miamala ya kifedha kati ya Tanzania na China kupitia mfumo wa malipo wa papo kwa papo.
Kupitia ushirikiano huo, KuwaPay itakuwa mdhamini rasmi wa kampeni zote za msimu wa pili wa filamu hiyo, ikiwemo uzinduzi rasmi, kampeni za kidijitali, mikutano na waandishi wa habari, shughuli za mazingira, programu za vyuo vikuu pamoja na maonesho ya filamu ndani na nje ya Tanzania.
Filamu ya Guardians of the Peak imeendelea kujijengea nafasi kama jukwaa la kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, kukuza utalii na kuwashirikisha vijana katika masuala ya maendeleo endelevu.
Msimu wa pili wa filamu hiyo unatarajiwa kuonyeshwa rasmi Agosti 22, 2026 nchini Tanzania kabla ya uzinduzi wa kimataifa nchini China, hatua inayotarajiwa kuongeza ushirikiano wa kiutamaduni, kibiashara na kiuwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande wa KuwaPay, ushirikiano huo unaipa kampuni fursa ya kuwafikia watalii, wawekezaji, wafanyabiashara, wanafunzi, wadau wa mazingira na jamii ya Wachina wanaofanya biashara au kuishi Tanzania.
Kampuni hiyo inaeleza kuwa mfumo wake unarahisisha malipo ya papo kwa papo kwa fedha za China, jambo linalowezesha biashara na miamala ya kuvuka mipaka kufanyika kwa usalama na ufanisi zaidi.
Mbali na udhamini, KuwaPay pia itatoa miundombinu ya malipo itakayosaidia shughuli za kimataifa za Guardians of the Peak, hususan katika kurahisisha miamala inayohusisha washirika na wadau waliopo China.
Wadau wa mradi huo wanasema ushirikiano huo unaonyesha jinsi sekta ya ubunifu na teknolojia ya kifedha zinavyoweza kushirikiana kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, kukuza utalii na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China.
Kupitia hatua hiyo, Guardians of the Peak inaendelea kupanua mtandao wake wa washirika wa kimkakati huku KuwaPay ikijijengea nafasi kama daraja la kidijitali linalounganisha biashara, watu na fursa kati ya Tanzania na China.
