Dkt. Bishanga: Malezi bora yanahitaji uwepo, si fedha pekee

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Daktari Dunstan Bishanga amesema baba wa leo anatakiwa kusawazisha jukumu la kutafuta kipato na jukumu la kulea familia, akisisitiza kuwa uwepo wa baba katika maisha ya watoto ni muhimu sawa na mahitaji ya kifedha.

Akizungumza katika mjadala kuhusu malezi ulioandaliwa na Empower Leaders Ministry  chini ya Taasisi ya Uongozi na Utafiti ya Diminion iliyopo Jijini Dar es Salaam, Dkt. Bishanga alisema mabadiliko ya maisha na shinikizo la kutafuta kipato yamewalazimu baadhi ya baba kufanya kazi kwa saa nyingi au mbali na familia zao.

"Kinachohitajika si uwepo wa muda mrefu pekee, bali uwepo wenye ubora. Familia inahitaji kujua kwamba baba yupo," alisema.

Alisema baba anatakiwa kujifunza hatua za makuzi ya mtoto na kuelewa mahitaji ya watoto pamoja na mwenzi wake ili aweze kutoa malezi yanayojenga kujiamini, kujithamini na kuimarisha uhusiano wa familia.

Kwa mujibu wake, malezi bora yanahitaji juhudi za makusudi za kutenga muda wa kuwa na watoto kila fursa inapopatikana.

Dkt. Bishanga alisema hata baba anayefanya kazi mbali anaweza kuendelea kuwa sehemu ya maisha ya familia kwa kuweka mawasiliano ya mara kwa mara.

"Malezi ni sehemu ya majukumu ya kila mzazi/mlezi. Yapange kwenye ratiba yako kama unavyopanga kazi nyingine," alisema.

Alisisitiza kuwa mawasiliano ya katikati ya wiki yanawapa watoto na mwenzi nafasi ya kueleza mahitaji yao na kumwezesha baba kutoa msaada na ushauri kwa wakati.

Kila baba anapopata nafasi ya kurejea nyumbani anapaswa kuitumia vizuri kwa kushiriki shughuli za familia na kutumia muda wa ubora na watoto.

"Hata kama ni masaa matatu tu ya quality time, mtoto anaweza kuyakumbuka kwa mwezi mzima. Muda huo unaweza kuwa na athari kubwa kuliko kuwa karibu kila siku bila kuwapa umakini," alisema.

Dkt. Bishanga alihitimisha kwa kuwataka akina baba kuona malezi kama uwekezaji wa maisha ya watoto, akisema uwepo wao leo unachangia kujenga kizazi chenye kujiamini, kinachojithamini na kinachowaamini wazazi wake.