Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amemtaka mkandarasi China Road and Bridge Corporation (CRBC) kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara chini ya Mradi wa Uboreshaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II).
Mhandisi Seff amesema Serikali haitavumilia ucheleweshaji wa miradi unaoweza kuwanyima wananchi huduma kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi katika wilaya za Ubungo na Kinondoni, alisema bado hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji katika baadhi ya maeneo.
"Mmeomba kuongezewa muda. Sasa ni lazima muongeze kasi, nguvu kazi na vifaa ili mkamilishe kazi kwa wakati," alisema.
Alionya kuwa endapo mkandarasi huyo hatatekeleza maelekezo hayo, Serikali inaweza kuchukua hatua kali ikiwemo kuvunja mkataba.
"Kinyume na hapo tutalazimika kuwapa kazi watu wenye uzoefu zaidi ili kulinda maslahi ya wananchi na Serikali," alisema.
Seff pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama katika maeneo ya ujenzi kwa kuweka alama za tahadhari ili kuwalinda watumiaji wa barabara.
Hata hivyo, aliipongeza CRBC kwa kukamilisha madaraja ya Msumi na Goba-Wakorea yaliyokuwa yakisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hasa kipindi cha mvua.
"Kukamilika kwa madaraja haya ni faraja kubwa kwa wananchi. Haya ni maeneo ambayo yalikuwa changamoto kwa muda mrefu," alisema.
Aidha, aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya miradi na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji.
Katika ziara hiyo, Seff alikagua miradi mbalimbali ya barabara na madaraja inayotekelezwa katika wilaya za Ubungo na Kinondoni chini ya DMDP II.
Mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya usafiri, kupunguza changamoto za usafirishaji na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wakazi wa Dar es Salaam.

