Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Winner Lukumay ni miongoni mwa wanawake waliokuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia wakati ajenda hiyo ikiwa bado haijapewa uzito mkubwa katika jamii.
Leo, anasema anaona matokeo ya safari hiyo. Si kwa mazingira pekee, bali pia kwa maisha ya wanawake wengi waliopata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi.
"Nilianza kama mwanamke wa kawaida nikiamini katika mabadiliko ya matumizi ya nishati. Tulihamasisha watu waondoke kwenye matumizi ya kuni na mkaa na waelekee kwenye nishati safi. Leo tunaona matokeo yake," alisema.
Winner anasema ushiriki wake katika kampeni za nishati safi ulimkutanisha na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, wakiwemo viongozi wa TZLPGA nchini.
Kupitia ushiriki huo, alipata nafasi ya kushiriki mijadala ya kitaifa na kimataifa kuhusu nishati safi, jambo ambalo limepanua upeo wake na kumwezesha kuendelea kuhamasisha jamii, na kuwa mratibu wa kitaifa wa wanawake na LPG.
"Nishati safi imenifungulia milango mingi. Lakini kikubwa zaidi, imenipa nafasi ya kuwafikia wanawake wengine na kuwaelimisha kuhusu faida zake," alisema.
Kwa mujibu wake, wanawake ndio watumiaji wakubwa wa nishati za kupikia majumbani, hivyo wana nafasi muhimu katika kuharakisha mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi.
"Tukiwafikia wanawake, tutakuwa tumeifikia jamii nzima. Ndiyo maana ninaamini wanawake wanaweza kuwa mabalozi wakubwa wa mabadiliko haya," alisema.
Winner anasema matumizi ya nishati safi siyo suala la teknolojia pekee, bali ni suala la afya, mazingira na maendeleo ya familia.
Aliwataka wanawake kujitokeza kujifunza na kutumia nishati safi kwa sababu inasaidia kupunguza madhara ya moshi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuokoa muda unaotumika kutafuta nishati za jadi.
"Ningependa kuona wanawake wengi zaidi wakishiriki katika ajenda hii. Tushirikiane, tuelimishane na tuwe sehemu ya mabadiliko yatakayowanufaisha watoto wetu na vizazi vijavyo," alisema.
Kadiri Tanzania inavyoendelea kusukuma matumizi ya nishati safi ya kupikia, simulizi za wanawake kama Winner Lukumay zinaonyesha kuwa mabadiliko makubwa huanza na mtu mmoja anayethubutu kuamini katika wazo jipya na kulisimamia.
