Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeibuka mshindi wa tuzo ya Muoneshaji Bora wa Taasisi za Serikali katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026.
Tuzo hiyo imepokelewa Julai 14 na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa REA, Martha Chassama, kwa niaba ya watumishi walioshiriki katika maonesho hayo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhandisi Saidy aliwapongeza watumishi wa REA kwa juhudi, kujituma na ushirikiano ulioiwezesha taasisi hiyo kupata ushindi.
"Tuzo hii ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na watumishi wetu. Nawapongeza kwa kujituma na kuiwakilisha vyema REA," alisema.
Aliwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano katika utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini na vitongojini.
Mhandisi Saidy alisema kuwa REA itaendelea kusukuma mbele agenda ya upatikanaji wa nishati kwa wananchi wote ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Ushindi huo unaongeza mafanikio ya REA katika juhudi zake za kusogeza huduma za nishati karibu na wananchi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini.