Mkuu wa Mkoa Tanga aipongeza TARURA kwa ubora wa barabara ya Lushoto

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amempongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, kwa usimamizi wa mradi wa barabara katika Wilaya ya Lushoto ambao umeelezwa kufikia viwango vya juu vya ubora.

Pongezi hizo alizitoa alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipatiwa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya TARURA.

Batilda alisema ujumbe wake wa pongezi ufikishwe kwa Mtendaji Mkuu wa TARURA kutokana na mafanikio ya mradi huo ambao ulitembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Alisema viongozi wa Mwenge wa Uhuru walifanya ukaguzi wa barabara hiyo na kuridhishwa na kiwango cha kazi kilichotekelezwa.

“Baada ya Mwenge kuipima barabara hiyo waliridhika kwa ubora wake na kuchukua sampuli ya lami (core) kwenda nayo kama mfano wa ubora wa ujenzi wa barabara,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, hatua hiyo inaonesha kuwa mradi huo umejengwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na kwamba unaweza kuwa mfano kwa miradi mingine ya miundombinu nchini.

Alisema mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa usimamizi madhubuti, matumizi ya wataalamu wenye sifa na ufuatiliaji wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

TARURA imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini nchini kwa lengo la kuboresha usafiri, kurahisisha huduma za kijamii na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali.