DAR ES SALAAM
Wanasayansi wamegundua kwa mara ya kwanza mfumo unaoitwa microblazar ndani ya galaksi ya Milky Way, ambao unaweza kuwa miongoni mwa vyanzo vyenye nguvu kubwa vya kuharakisha chembe angani.
Ugunduzi huo umefanywa na timu ya wataalamu wa anga kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo ASTRON na Chuo Kikuu cha Amsterdam.
Microblazar hiyo, iliyopewa jina IRAS 18293−0941, inaundwa na black hole yenye uzito unaokadiriwa kuwa mara 10 ya Jua pamoja na nyota kubwa inayozunguka nayo.
Black hole hiyo inatoa mkondo mkubwa wa nishati unaoelekea upande wa Dunia. Mkondo huo unapogonga wingu la gesi na vumbi lililopo angani, husababisha chembe kuharakishwa hadi karibu na kasi ya mwanga.
Wanasayansi wanakadiria kuwa nishati inayozalishwa inaweza kufikia petaelectronvolts, kiwango cha juu sana cha nishati ya chembe. Nguvu hiyo ya kuharakisha chembe inaweza kuwa karibu mara 100 zaidi ya Large Hadron Collider (LHC), mashine kubwa inayotumiwa na wanasayansi kuchunguza chembe.
Ugunduzi huo unaweza kusaidia kueleza chanzo cha baadhi ya chembe zenye nishati kubwa zinazofika Duniani kutoka angani, ambazo zimekuwa zikichunguzwa kwa zaidi ya karne moja huku asili yake ikiwa bado ni miongoni mwa maswali makubwa katika sayansi ya anga.
Wataalamu wameutambua mfumo huo kwa kutumia taarifa kutoka kwenye darubini za redio, X-ray, gamma ray na infrared. Ingawa ulirekodiwa tangu mwaka 1983, uchunguzi mpya umewezesha kuelewa kwa undani zaidi shughuli zinazotokea ndani yake.
Mtafiti Benito Marcote amesema ugunduzi huo unaweza kusaidia wanasayansi kuelewa zaidi namna blazar kubwa zilizo mbali katika galaksi nyingine zinavyofanya kazi.
Wataalamu wanaendelea kuchunguza eneo ambalo mkondo wa black hole unapogongana na wingu la gesi. Utafiti huo umechapishwa katika jarida la Astronomy & Astrophysics.
