New york, Marekani:
Tanzania imetangaza azma ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kwa kipindi cha 2029–2030, ikiahidi kupeleka sauti ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.
Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Amesema Tanzania ikichaguliwa itatoa kipaumbele kwa kuzuia migogoro kabla haijawa vita, kuongeza nafasi ya wanawake na vijana katika ulinzi na ujenzi wa amani, pamoja na kuimarisha operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani. Dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.
Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa mageuzi katika Umoja wa Mataifa ili kuimarisha haki, usawa na uwakilishi wenye uwiano, hasa wakati dunia ikikabiliwa na migogoro na vita, mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, maendeleo ya Akili Mnemba (AI) na changamoto za usalama wa nishati. Pia imeitaka nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika taasisi za fedha duniani na kusisitiza upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu, fedha za maendeleo na tabianchi pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi.
Akizungumzia afya ya mama na mtoto, Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imeongeza kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. Amesema Tanzania imepunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba na inalenga kufikia malengo ya “Sifuri Tatu”, ambayo ni kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. Amesema kufikia malengo hayo kunahitaji uongozi thabiti, rasilimali za kutosha na ushirikiano wa kimataifa.
Katika eneo la mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi wa kugharamia hatua za kukabiliana na athari zake. Tanzania imetaja Bwawa la Julius Nyerere lenye uwezo wa megawati 2,115, miradi ya jua na upepo yenye megawati 650, mipango ya megawati 130 za jotoardhi, reli ya umeme na lengo la kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika asilimia 80 ya kaya ifikapo 2034.
Kuhusu diplomasia ya kimataifa, Tanzania imepinga matumizi ya vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi nyingine na kueleza mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo. Kuhusu Gaza na Mashariki ya Kati, imesisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji na kurejesha diplomasia kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu.
Kwa ujumla, Tanzania imesema safari yake ya kuwania kiti katika Baraza la Usalama la UN inalenga kuimarisha sauti ya Afrika, kuzuia migogoro, kutetea suluhu za amani na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa ili uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi.


