Abu Dhabi, UAE
Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), jijini Abu Dhabi, ambako amesaini kitabu cha wageni na kufanya mazungumzo na maafisa wa ubalozi huo.
Ziara hiyo imefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Nishati wa ADIPEC 2026, unaofanyika kuanzia Novemba 2 hadi 5, mwaka huu, ukiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kujadili changamoto na fursa katika sekta hiyo.
Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo ni usalama wa nishati, mnyororo wa ugavi wa nishati pamoja na matumizi ya akili unde (AI) katika shughuli mbalimbali za sekta hiyo.
Kupitia jukwaa hilo, Tanzania imetumia fursa hiyo kutangaza miradi mbalimbali ya nishati inayotekelezwa nchini, ikiwemo miradi ya mafuta na gesi asilia, umeme na nishati jadidifu, kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kukuza uwekezaji katika sekta hiyo.
Dkt. Homera amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini UAE, Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed, pamoja na maafisa wa ubalozi.
