DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba J.A. Kabudi, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), baada ya maambukizi mapya kupungua kutoka watu 68,754 mwaka 2010 hadi 33,511 mwaka 2025.
Aidha, amesema vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua kutoka watu 55,833 hadi 25,993 katika kipindi hicho, hatua inayoonesha mafanikio yaliyopatikana katika juhudi za kudhibiti ugonjwa huo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka 2026, Profesa Kabudi amesema mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo ya juhudi za Serikali na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yataanza Novemba 24 hadi Desemba Mosi, 2026, jijini Dodoma, sambamba na kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Ameeleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni "Ending AIDS Starts with Access", inayosisitiza kuwa huduma bora za afya ni msingi wa kutokomeza UKIMWI kupitia kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, shughuli za maadhimisho zitaanzia katika kanda saba za TACAIDS kuanzia Novemba 24, zikihusisha utoaji wa elimu, uhamasishaji na huduma mbalimbali za afya zinazohusiana na VVU na UKIMWI.
Amesema maadhimisho ya kitaifa yataanza Novemba 29 katika viunga vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Convention Centre (JICC), yakihusisha maonesho ya wadau wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, pamoja na utoaji wa huduma za afya na elimu kwa jamii.
Katika hatua nyingine, amesema maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 6.2, ikiwa ni hatua muhimu katika kulinda afya ya mama na mtoto.
Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya ya VVU, huku vijana wa kike wakichangia asilimia 77.7 ya maambukizi mapya katika kundi hilo.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund) kwa lengo la kuongeza vyanzo vya ndani vya fedha vitakavyosaidia kugharamia na kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Katika kuhitimisha, wananchi, viongozi wa ngazi mbalimbali, asasi za kiraia, sekta binafsi na vyombo vya habari wametakiwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, kupinga unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU na kuunga mkono juhudi za Serikali za kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

