Kombo ataka ushirikiano wa Nordic kuimarisha teknolojia na uwekezaji madini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amezitaka nchi za Nordic kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika uwekezaji, uhawilishaji wa teknolojia na mafunzo ya wataalamu ili kuongeza thamani ya madini na kupanua fursa za ajira nchini.

Kombo ametoa wito huo Novemba 19, 2026, jijini Oslo, Norway, wakati wa majadiliano kuhusu Minyororo Endelevu ya Thamani ya Madini ya Kimkakati, yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Nordic na Afrika.

Akizungumzia msimamo wa Tanzania kuhusu uongezaji thamani wa madini, amesema Serikali imeweka katika sheria matakwa ya kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanafanyiwa uchakataji kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, angalau katika hatua za awali.


Hata hivyo, amesema changamoto inayokabili juhudi hizo ni upatikanaji wa teknolojia za kisasa za uchakataji, kutokana na baadhi ya kampuni za kimataifa kulinda hataza na teknolojia wanazomiliki.

Amesema Serikali inaendelea kutafuta suluhisho kwa kuhakikisha wawekezaji wanaoingia nchini wanatoa mafunzo ya kitaalamu kwa Watanzania, ili kuwawezesha kupata ujuzi na kushiriki katika shughuli za uchakataji wa madini.

Kombo ameeleza kuwa nchi za Nordic zina nafasi ya kusaidia juhudi hizo kupitia uwekezaji, teknolojia na utaalamu katika uchimbaji endelevu na wenye uwajibikaji, hatua itakayosaidia kukuza viwanda na kuongeza manufaa ya rasilimali za madini kwa wananchi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika kubadilishana ujuzi na teknolojia ili kuimarisha uwezo wa bara hilo katika kuendeleza minyororo ya thamani ya madini ya kimkakati.