Morogoro.
Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT) limefikia zaidi ya wakulima, wafugaji, maafisa ugani na wadau 450,000 katika kipindi cha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, likichangia mabadiliko ya uzalishaji, ukuaji wa kipato cha wakulima na uhifadhi wa mazingira kupitia mifumo ya kilimo hai na ikolojia.
Mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo yaliyowasilishwa na shirika hilo wakati wa kuadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, yakionesha pia kufikiwa kwa zaidi ya vijiji 700 katika kata 285, wilaya 30 na mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na kuunga mkono zaidi ya vikundi 3,000 vya wakulima.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa SAT, Janet Maro, alisema shirika hilo lilianza shughuli zake Mei 2011 na kusajiliwa rasmi Juni 6, mwaka huo, likiwa halina ofisi wala eneo lake la kufanyia kazi, lakini limeendelea kukua na sasa lina majengo, ofisi katika maeneo mbalimbali na zaidi ya wafanyakazi 80.
Alisema katika safari hiyo, SAT imeshiriki pia katika kuimarisha sera za kilimo nchini, ikiwemo mchakato wa kuingiza vipengele vya kilimo hai katika Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 na juhudi za kuanzishwa kwa Mkakati wa Kitaifa wa Kilimo Ikolojia Hai uliozinduliwa mwaka 2023.
Katika eneo la elimu na utafiti, shirika hilo limechangia kuboresha zaidi ya mitaala 21 inayotumika katika vyuo zaidi ya 55 vinavyotoa mafunzo ya ngazi ya kati nchini, huku zaidi ya taasisi 120 zikipewa mafunzo kuhusu mbinu za kilimo ikolojia.
Kwa upande wa mazingira, takwimu za SAT zinaonesha kuwa zaidi ya miti milioni 12 imepandwa na zaidi ya ekari 150,000 za ardhi zimerejeshwa katika hali nzuri. Aidha, migogoro imepungua kwa asilimia 88 katika jamii 80 zilizofikiwa na shughuli za shirika hilo.
Matokeo hayo yanaonekana pia katika uchumi wa wakulima, ambapo kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 49 ya wakulima walioripoti matokeo ya shughuli zao wameonesha ukuaji wa kipato wa hadi asilimia 67, huku asilimia 51 wakiripoti ongezeko la mavuno la hadi asilimia 266.
Aidha, SAT imeunga mkono biashara ndogo na za kati 57, kuwezesha kuanzishwa kwa biashara zaidi ya 760, maduka saba ya bidhaa za kilimo hai katika mikoa minne na kampuni 11 zinazofanya biashara ya bidhaa za kilimo hai katika masoko ya kimataifa. Shirika hilo pia limewezesha kuanzishwa kwa maghala manne ya mazao, vituo vinne vya usindikaji na vyama vya ushirika saba.
Katika kuwawezesha wakulima kiuchumi, zaidi ya Sh bilioni 1.5 huzunguka kila mwaka kupitia mikopo midogo inayotolewa kwa wakulima na wafugaji, hatua inayosaidia kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na ujasiriamali.
Akitoa ushuhuda wa ushirikiano wake na SAT, Mzee Pius Paulin mmoja wa wakulima aliyeshirikiana na shirika hilo kwa miaka 15, alisema mwanzoni haikuwa rahisi kwa mkulima mdogo kukaa pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kujadili changamoto za kilimo, lakini sasa ushirikiano huo umeimarika na kuwawezesha kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili.
Alisema ushirikiano huo umewafungulia wakulima fursa za kujifunza mbinu bora za kilimo, ikiwemo baadhi yao kupata nafasi ya kutembelea nchi nyingine kama Kenya kwa ajili ya kubadilishana uzoefu. Alisisitiza kuwa uzalishaji wa chakula salama ni msingi wa afya na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Msakuzi iddi msakuzi alisema alijiunga na SAT mwaka 2018 kama mwezeshaji wa vikundi vya wakulima na kwamba mafunzo aliyopata kuhusu matumizi ya mbolea na dawa za asili yamemwezesha kuwafundisha wakulima wengine na kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka Kinole, Barnabas Ndangalari, alisema SAT imechangia kwa kiasi kikubwa kubadili mtazamo wa wakulima kuhusu shughuli za kilimo, hususan kwa kuongeza uelewa na hamasa ya matumizi ya mbolea na viuatilifu vya asili katika uzalishaji.
Alisema elimu inayotolewa na shirika hilo imekuwa chachu ya kuwahamasisha wakulima kuachana na baadhi ya mbinu zisizo rafiki kwa mazingira na kuzingatia njia endelevu zinazolinda afya ya binadamu na kuboresha ubora wa mazao.
Katika kuendeleza mafanikio hayo, SAT imeanzisha miradi mipya mwaka 2026/27 inayolenga kuboresha lishe shuleni katika mikoa ya Morogoro na Dodoma, kujenga mabwawa ya mchanga katika Chemba na Kongwa kwa ajili ya kuhifadhi maji, pamoja na kulinda na kuendeleza mbegu na mazao ya asili yasiyopewa kipaumbele katika kata ya Kongwa, Chamwino na Mpwapwa.
Katika eneo la miundombinu, shirika hilo limeonesha mafanikio ya kuanzisha matanki 160 ya kuvuna maji ya mvua, miradi 90 ya upatikanaji wa maji na miundombinu, mifumo minne ya umwagiliaji iliyofanyiwa maboresho, mabwawa saba yaliyojengwa na mawili yaliyokarabatiwa.
Katika maadhimisho hayo, SAT ilitoa zawadi kwa watu watano waliotambuliwa kwa mchango wao chanya kwa shirika, kila mmoja akipatiwa Sh milioni 1.5. Pia vikundi vya wakulima, vijana, wanawake na wafugaji vilitambuliwa na kupewa zawadi kutokana na kufanya vizuri katika uongozi, ujasiriamali, utunzaji wa akiba, ubunifu na uendelevu wa shughuli zao.
Miongoni mwa vilivyotambuliwa ni Umoja ni Nguvu Misala, kilichopata Sh 150,000 baada ya kufikisha akiba ya zaidi ya Sh milioni 71, huku katika ukanda wa viungo vikundi vikifikisha akiba ya Sh milioni 36, ambapo Mishujadi Hinda kiliongoza kwa kufikisha Sh milioni 13. Mbikamu SACCOS ya Mlowa, wilayani Chemba, Dodoma, pia ilizawadiwa Sh 100,000 kwa juhudi zake za kuweka akiba na kuanza ujenzi wa ofisi kwa nguvu zake.
Kwa upande wa wafanyakazi, baadhi yao walieleza kuridhishwa na mazingira ya kazi, ushirikiano na fursa za kujifunza walizopata ndani ya shirika hilo, wakibainisha kuwa SAT imekuwa sehemu muhimu ya kukuza taaluma zao na kuwawezesha vijana kujitegemea kupitia miradi mbalimbali.
Maadhimisho hayo yalikuwa fursa ya kutambua mchango wa wakulima, wafanyakazi, wadau na vikundi mbalimbali katika safari ya shirika hilo, huku SAT ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kilimo hai katika kuimarisha uchumi wa wakulima, afya za jamii na uhifadhi wa mazingira.




