Na Mwandishi wetu, Mbeya
TANESCO imesema inalenga kurejesha huduma ya umeme katika mikoa ya Mbeya na Songwe kufikia Jumapili usiku, Novemba 22, baada ya kuanguka kwa mnara wa kusafirisha umeme kusababisha kukatika kwa huduma katika maeneo hayo.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO anayeshughulikia Usafirishaji Umeme, Mhandisi Zakaria Mhagama, amesema mafundi wanafanya kazi ya kuandaa njia mbadala ya kusafirisha umeme ili kurejesha huduma wakati matengenezo yakiendelea.
Amesema hitilafu hiyo ilitokea Jumamosi, Novemba 21, majira ya saa 9:21 alasiri, baada ya njia mpya ya umeme iliyokuwa imejengwa kupata hitilafu na kuangukia njia ya zamani inayosafirisha umeme kutoka Makambako kwenda Mbeya.
Mha. Mhagama amesema timu za wataalamu zilifika eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali hiyo na kuanza kazi ya kutafuta namna ya kurejesha umeme kupitia mfumo mwingine mbadala.
Ameomba radhi kwa wananchi walioathirika na kukatika kwa huduma hiyo, akisema TANESCO inaendelea na juhudi za kuhakikisha umeme unarejea haraka.
Kwa mujibu wa taarifa ya TANESCO iliyotolewa Jumapili, mnara ulioanguka ni sehemu ya njia mpya ya kilovoti 400 inayojengwa kupitia mradi wa Tanzania-Zambia Transmission Interconnector (TAZA). Tukio hilo pia lilisababisha uharibifu katika miundombinu ya njia ya zamani ya kilovoti 220 inayounganisha Iringa na Mbeya.
TANESCO imesema mafundi wanaendelea na kazi ya kurejesha huduma na itaendelea kutoa taarifa kuhusu hatua zinazofikiwa.
Mradi wa TAZA ni sehemu ya uwekezaji wa Tanzania katika miundombinu ya kusafirisha umeme kwa msongo mkubwa, ukiwa na lengo la kuimarisha gridi ya taifa na kuwezesha muunganiko wa umeme kati ya Tanzania na Zambia.
TANESCO imewaomba wananchi kuwa na subira wakati kazi za dharura zikiendelea.


