TANESCO yajenga njia mbadala kupunguza changamoto ya umeme maeneo manne

Wateja wa umeme katika maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti wanatarajiwa kupata nafuu ya huduma baada ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga njia mbadala ya muda ya kusafirisha umeme kwa njia ya juu, kufuatia hitilafu iliyotokea kwenye miundombinu ya chini ya ardhi eneo la Gongolamboto.

Njia hiyo mpya imejengwa ili kufidia sehemu ya njia ya kilovoti 132 iliyoharibika na kuvuka eneo la miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR), hatua inayolenga kuendelea kusafirisha umeme kwa wateja wakati matengenezo ya njia ya chini ya ardhi yakiendelea.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema hayo Novemba 7, 2026, wakati akikagua maendeleo ya kazi za matengenezo na kupongeza wataalamu wa shirika hilo kwa kubuni na kutekeleza suluhisho hilo la dharura kwa haraka.

Amesema shirika linaendelea kuchukua hatua za kiufundi kuhakikisha wateja wanapata huduma ya umeme wakati wote, huku akiwahakikishia kuwa jitihada za kurejesha hali ya kawaida zinaendelea. Pia amewashukuru wateja kwa uvumilivu wao katika kipindi cha changamoto hiyo.

Twange amesema TANESCO itaendelea kuimarisha miundombinu na kutafuta njia za kupunguza athari kwa wateja pale hitilafu za kiufundi zinapotokea, akisisitiza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuridhika kwa wateja ni vipaumbele vya shirika.

Kwa upande wao, wataalamu wa TANESCO wanaendelea na kazi za kuunganisha na kukamilisha mfumo huo mbadala, wakizingatia taratibu za usalama ili kuhakikisha unakuwa tayari kutumika kwa ufanisi.

Hitilafu hiyo ilianza Novemba 3, 2026, kwenye njia ya kilovoti 132 inayounganisha Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Gongolamboto na vituo vya Mbagala na Dege, Kigamboni. Changamoto hiyo iliathiri upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo pamoja na Mkuranga na Kibiti, baada ya njia mbadala iliyokuwepo awali kushindwa kubeba mahitaji yote ya umeme kwa wakati mmoja.