Mradi wa umeme Mkuranga–Mafia kufungua fursa za uchumi

Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kupitia mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 33 kutoka Mkuranga hadi Kisiwa cha Mafia kwa njia ya waya maalumu itakayopita chini ya bahari.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omary Said, amesema mradi huo utachangia kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za uzalishaji, hususan katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.

Amesema uongozi wa wilaya utaendelea kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa ubora na bila vikwazo vinavyoweza kuchelewesha kukamilika kwake. Pia amewapongeza TANESCO kwa juhudi za kupanua huduma ya umeme kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Mradi, Mhandisi Joffrey Katoto amesema mradi huo wa kupeleka umeme Zanzibar na Mafia una thamani ya dola za Marekani milioni 283 na unahusisha njia tatu za usafirishaji wa umeme.

Amezitaja njia hizo kuwa ni Mkuranga hadi Mafia yenye kilovoti 33, Tanga hadi Pemba yenye kilovoti 132 na Ununio hadi Unguja yenye kilovoti 220.

Katika hatua ya maandalizi, TANESCO imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi na viongozi wa vijiji kuhusu njia itakayopitiwa na mradi, maeneo yatakayoathiriwa pamoja na utaratibu wa kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji. Baadhi ya washiriki wamesema elimu hiyo imewasaidia kuelewa maeneo husika na namna ya kushughulikia masuala yatakayojitokeza.

Semina hizo pia zinalenga kuimarisha ushirikiano kati ya TANESCO, viongozi wa Serikali na wananchi, pamoja na kuwajengea viongozi wa maeneo husika uwezo wa kutatua kwa haraka migogoro inayoweza kujitokeza ili kurahisisha utekelezaji wa mradi.