Uwekezaji katika uzalishaji na uchakataji wa maziwa mkoani Iringa umevutia Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za sekta hiyo.
Baada ya kutembelea shamba la mifugo na kiwanda cha ASAS, Dkt. Bashiru amewataka wafugaji kuzingatia misingi ya sayansi na utaalamu ili kuboresha uzalishaji na kuifanya sekta ya mifugo kuwa ya kibiashara. Amesema wataalamu waliopo nchini wana ujuzi unaopaswa kuheshimiwa na kupewa nafasi pamoja na nyenzo za kutekeleza majukumu yao.
Pia ameipongeza ASAS kwa kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua na kutumia ardhi kwa uzalishaji wa malisho ya mifugo, akisema hatua hizo zinaendana na maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifugo inapata chakula na maji ya kutosha.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika, amesema uwekezaji huo umeongeza hamasa kwa kamati katika jukumu lake la kuishauri Serikali kuhusu namna bora ya kuendeleza sekta ya maziwa. Amesema matumizi ya ardhi yaliyofanywa na ASAS ni mfano unaopaswa kuigwa, akibainisha kuwa kampuni nyingi zenye uwekezaji wa aina hiyo zingeweza kuleta maendeleo makubwa nchini.
Mkurugenzi wa kiwanda cha ASAS, Fuad Jaffer, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano, akieleza kuwa mbali na uzalishaji wa maziwa, kampuni hiyo ina mpango wa kuzalisha mitamba ili kuwasaidia wafugaji wanaohitaji ng'ombe bora wa maziwa.
Katika ziara hiyo, viongozi hao pia walitembelea shamba la mifugo na kiwanda cha kusindika maziwa cha Shafa pamoja na shamba la mwekezaji Richard Philips, maarufu kama Kibebe. Philips ameishukuru Serikali kwa kuwapatia chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng'ombe.
Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Maziwa yanayofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa, Iringa, ambayo yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 1, 2026.
