Vijana wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wanatarajiwa kunufaika na fursa za ufadhili wa elimu ya juu kupitia ushirikiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Ushirikiano huo unalenga kuwawezesha vijana kupata elimu na ujuzi katika fani mbalimbali zitakazowaongezea uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo, uhifadhi wa mazingira na kukuza uchumi wa jamii inayozunguka hifadhi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill M. Kiwia, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kupanua upatikanaji wa elimu ya juu, hasa kwa vijana wenye uhitaji wa kifedha. Amesema bodi itaendelea kusimamia ufadhili kwa kuzingatia uwazi, usawa, uwajibikaji na haki ili wanafunzi wenye sifa wapate nafasi zinazostahili.
Mratibu wa Miradi kutoka HESLB, Gertrude Alphonce, amesema mpango huo una vigezo maalumu vinavyotaka mnufaika awe raia wa Tanzania, awe ameishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa kipindi kisichopungua miaka minne na athibitishe kuwa na uhitaji wa kifedha.
Amesema maombi ya ufadhili yatapokelewa na kuchakatwa kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo wa Digital Exam Solutions au akaunti za taasisi husika, hatua inayolenga kuimarisha uwazi na uadilifu katika mchakato wa kupata wanufaika.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Abdul-Razaq Badru, amesema elimu katika fani za usimamizi wa wanyamapori, utalii na ukarimu itawasaidia vijana kupanua shughuli zao za kiuchumi na kupunguza utegemezi wa ufugaji wa jadi pekee.
Amesema ushirikiano wa Serikali na wadau unapaswa kuimarishwa ili kuongeza upatikanaji wa rasilimali, mikopo na fursa nyingine za kuwawezesha wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha makundi mbalimbali yanashirikishwa katika fursa za maendeleo.
