Na Mwandishi wetu
TANZANIA inahitaji jumla ya dola za Marekani bilioni 19.3 kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC 3.0), huku Serikali ikiwa tayari imepata ahadi na fedha zenye thamani ya dola bilioni 7.3.
Hata hivyo, kiasi cha dola bilioni 12 bado kinahitaji kupatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya ufadhili ili kuwezesha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa katika mpango huo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Uturuki.
Amesema Oktoba 5, Wizara ya Fedha ilikutana na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kujadili mikakati ya kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Katika jitihada hizo, sekta ya fedha na taasisi binafsi zimeendelea kuhamasishwa kushiriki katika uwekezaji wa miradi inayolenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Benki ya CRDB ni miongoni mwa taasisi zilizochukua hatua katika eneo hilo kupitia utoaji wa hati fungani za kijani (Green Bonds), zinazolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu.
Aidha, juhudi nyingine zinaelekezwa katika kupunguza matumizi ya nishati chafu na kuhamasisha matumizi ya usafiri wa umeme pamoja na nishati safi ya kupikia.
Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kusaidia Tanzania kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari zake kwa wananchi na kuimarisha maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
