Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam, Tanzania imefanikiwa kupata ufadhili wa dola za kimarekani milioni 120, sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 318, kwa ajili ya kukamilisha mradi wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria hadi mkoani Simiyu, pamoja na kuteuliwa kuwa kitovu cha mafunzo na mikutano ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.
Mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo ya diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali kupitia ushirikiano na wadau wa kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kuhusu mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Uturuki, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Stanslaus Muyungi, amesema Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Dunia umekubali kutoa fedha zote zinazohitajika kukamilisha mradi huo wa maji.
Amesema ziara hiyo ilihusisha ushiriki wa Rais Samia katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), uliofanyika Antalya, Uturuki.
Ameeleza kuwa mradi huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 125 unatarajiwa kunufaisha zaidi ya kaya 500,000 katika vijiji 103 mkoani Simiyu.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za kidiplomasia za Rais Samia ambazo zimewezesha kufikiwa kwa makubaliano ya ufadhili wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Tanzania imepata fursa ya kuwa kitovu cha Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) kwa ajili ya mafunzo ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa vijana wa Afrika, ambapo jengo maalumu linatarajiwa kutafutwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli hizo.
Aidha, Tanzania na Misri zimeteuliwa kuwa vituo vikuu vya mikutano ya Afrika inayohusu mabadiliko ya tabianchi, huku Tanzania ikitarajiwa kuhudumia nchi za ukanda wa Afrika zinazotumia lugha ya Kiingereza.
Mkataba rasmi wa makubaliano hayo unatarajiwa kusainiwa kati ya Waziri mwenye dhamana na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.
Vilevile, Tanzania imepata fursa ya kuandaa mafunzo ya kimataifa ya matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mwaka ujao, kufuatia mafanikio ya binti wa Kitanzania, Upendo Limo, aliyetunukiwa tuzo ya mshindi wa kwanza katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Katika eneo la uwekezaji, Tanzania imefanikiwa kuvutia wawekezaji katika biashara ya Kaboni kupitia ushiriki wa taasisi za fedha za ndani zikiwemo Benki ya CRDB na NMB, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC).
Wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo usafirishaji, viwanda, misitu na kilimo, huku taasisi moja ikikubali kuwekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 150 katika sekta ya kilimo.
Uwekezaji huo unatarajiwa kusaidia wakulima kunufaika na fursa za biashara ya kaboni, kuongeza uzalishaji na kupanua fursa za ajira kwa vijana.
