Tanzania yavutia uwekezaji wa Uturuki wa Trilioni 3.45

Na Mwandishi wetu

TANZANIA imevutia mpango wa uwekezaji wenye thamani ya dola za kimarekani Bilioni 1.3 ( sawa na Shilingi Trilioni 3.45) kutoka kampuni moja ya kituruki kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza Nishati Safi.

Mpango huo ni miongoni mwa matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Uturuki, inayolenga kuimarisha diplomasia ya uchumi, kukuza biashara na kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya ziara hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ng'waru Jumanne Maghembe (Mb.), amesema ziara hiyo imefungua fursa mpya za uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Amesema katika ziara hiyo, Rais Samia aliongoza ujumbe wa viongozi na wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Nne wa Nchi za COMCEC, uliofanyika Novemba 11 na 12 nchini Uturuki.

Katika mkutano huo, Tanzania ilieleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika upatikanaji wa fedha za maendeleo, uwekezaji katika Nishati Safi na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Aidha, Rais Samia aliwasilisha fursa za uwekezaji zilizopo nchini katika sekta za Chai, Kahawa, Tumbaku, Mbaazi, bidhaa za viwandani na Madini, huku akihamasisha wawekezaji kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Katika hatua nyingine, mazungumzo yaliyofanyika kati ya Rais Samia na viongozi wa kampuni mbalimbali za Uturuki kutoka Dar es Salaam na Ankara yalilenga kuimarisha biashara baina ya nchi hizo ili kuongeza uwiano wa kibiashara na kukuza uchumi wa pande zote mbili.

Serikali imeeleza dhamira ya kuhakikisha fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa zinazopatikana zinageuzwa kuwa miradi halisi itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.