Wiki hii, vyombo vya habari vya Marekani na kwingineko duniani viliandika kuwa maafisa wa CIA walihusika katika operesheni za siri zilizolenga viongozi wa cartel, ikiwemo mashambulizi yaliyosababisha vifo vya baadhi ya washukiwa wa biashara ya dawa za kulevya.
Ripoti hizo zilidai operesheni hizo zilihusisha kitengo maalum cha CIA kinachojulikana kama Ground Branch.
Lakini serikali ya Mexico pamoja na CIA zimekanusha vikali taarifa hizo.
Waziri wa Usalama wa Mexico, Omar Garcia Harfuch, alisema serikali “inakataa kabisa” madai yanayoonyesha kuwa mashirika ya kigeni yanafanya operesheni za siri au mashambulizi ya moja kwa moja ndani ya ardhi ya Mexico.
CIA nayo ilitoa taarifa ikisema madai hayo ni “ya uongo na hatari.”
Mjadala huo umeongezeka baada ya taarifa kwamba maafisa wawili wa Marekani waliodaiwa kuwa na uhusiano na CIA walifariki kwenye ajali ya gari nchini Mexico baada ya operesheni dhidi ya maabara ya dawa za kulevya katika jimbo la Chihuahua mwezi uliopita.
Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, amesema serikali yake haikutoa ruhusa kwa maafisa wa Marekani kushiriki moja kwa moja katika operesheni za kijeshi au za usalama ndani ya nchi hiyo.
Kwa upande mwingine, Marekani imeendelea kuongeza shinikizo dhidi ya cartel za Mexico kutokana na biashara ya fentanyl na dawa nyingine zinazochangia vifo vya maelfu ya watu nchini Marekani kila mwaka.
Wachambuzi wa usalama wanasema mvutano huu unaonyesha jinsi vita dhidi ya cartel sasa vinavyoingia kwenye hatua mpya inayochanganya ujasusi, siasa na operesheni za kimataifa.
Lakini hadi sasa, hakuna ushahidi rasmi uliowekwa wazi hadharani kuthibitisha kuwa CIA ilishiriki moja kwa moja katika mashambulizi ya kuwaua wanachama wa cartel ndani ya Mexico.
