Mtwara Yafungua Fursa Mpya Kwenye Biashara Ya Chumvi Tanzania

Mkoa wa Mtwara unaendelea kujitengenezea nafasi mpya kwenye biashara ya chumvi huku uzalishaji ukiongezeka na wawekezaji kuziona fursa hizo.

Ukuaji huo unachangiwa na mazingira mazuri ya uzalishaji, matumizi ya teknolojia pamoja na hatua ya Serikali kupunguza gharama za leseni za madini chumvi.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Winnifrida Mrema amesema sekta hiyo inaendelea kukua kwa kasi huku ikitoa ajira na kuongeza mapato kwa wananchi.

“Mtwara ina mazingira rafiki kwa uzalishaji wa chumvi na Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta hii,” amesema.

Katika Kijiji cha Mnete wilayani Mtwara Vijijini, mashamba ya chumvi yanayomilikiwa na Zamda Khatibu yanaendelea na maandalizi ya msimu mpya wa uzalishaji baada ya mvua.

Msimamizi wa mashamba hayo, Salum Amani amesema eneo hilo lina majaruba 24 ya uzalishaji pamoja na leseni mbili za uvunaji chumvi.

Amesema kwa kawaida majaruba manne huzalisha takribani tani 90 za chumvi kwa msimu mmoja, huku shughuli hizo zikitoa ajira kwa watu tisa katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa wazalishaji, jua kali husaidia chumvi kukauka ndani ya siku 30, lakini hali ya baridi inaweza kuongeza muda hadi siku 40.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Mkoa wa Mtwara, Khalfan Nassoro amesema kupunguzwa kwa ada ya leseni kutoka TZS 45,000 hadi TZS 20,000 kumeongeza matumaini kwa wachimbaji wadogo na wawekezaji.

Amesema gharama hizo mpya zinawapa nafasi wazalishaji wengi kuongeza maeneo ya uzalishaji na kuwekeza zaidi kwenye biashara ya chumvi.

Wadau wa sekta hiyo wanaamini ukuaji wa uzalishaji unaweza kusaidia kujengwa kwa viwanda vya kuongeza thamani ya chumvi, jambo litakaloongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi wa taifa.

Soma