NCMC yawataka waandishi kuelimisha umma kuhusu biashara ya hewa ukaa


Na Charles Mkoka

Serikali imeongeza juhudi za kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika biashara ya hewa ukaa huku vyombo vya habari vikitakiwa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.

Hayo yameelezwa katika mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Kituo cha Taifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu biashara ya hewa ukaa nchini.

Viongozi wa NCMC wamesema Tanzania inaendelea kujipanga kunufaika zaidi na masoko ya kimataifa ya hewa ukaa ambayo yanazidi kukua duniani.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji, Uhakiki, Usajili na Tathmini ya Gesijoto wa NCMC, Ndeo Shirima, amesema biashara ya hewa ukaa inahusisha shughuli zinazosaidia kupunguza au kuzuia hewa zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

Amesema biashara hiyo haihusiani na misitu pekee, bali pia na sekta za taka, nishati, viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Kila mtu anaweza kushiriki kwenye biashara hii, iwe kampuni, kikundi au mtu mmoja mmoja, mradi afuate taratibu zilizowekwa,” amesema Shirima.

Kwa mujibu wa Shirima, hadi sasa yapo makampuni takribani 99 yaliyo kwenye hatua mbalimbali za usajili wa miradi ya hewa ukaa nchini.

Amesema kati ya hayo, makampuni manane tayari yameanza utekelezaji wa miradi yao.

Shirima amesema biashara ya hewa ukaa inaweza kusaidia kuongeza mapato kwa wananchi na jamii zinazoshiriki kuhifadhi mazingira.

Ametoa mfano wa wananchi wa Wilaya ya Tanganyika waliopata zaidi ya Tshs bilioni 14 mwaka 2024 kupitia shughuli za usimamizi wa misitu zinazohusiana na biashara hiyo.

Baadhi ya wadau waliohudhuria mafunzo hayo wamesema bado kuna uelewa mdogo kwa wananchi kuhusu biashara hiyo na namna ya kunufaika nayo.

“Watu wengi bado hawajui biashara ya kaboni ni nini. Elimu zaidi inahitajika hasa vijijini,” amesema mmoja wa washiriki.

NCMC imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.

Taasisi hiyo sasa ina makao yake makuu Dodoma baada ya kuhamishwa kutoka Morogoro na kupewa hadhi kamili ya taasisi ya serikali.