Serikali, Boys Initiative wahamasisha uwekezaji kwa mtoto wa kiume


Na Mwandishi Wetu

Taasisi ya Boys Initiative Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imezindua rasmi kaulimbiu ya kitaifa ya Siku ya Mtoto wa Kiume Duniani 2026.

Kaulimbiu hiyo inasema, “Wekeza kwa mtoto wa kiume; kwa kizazi chenye uwajibikaji.”

Kampeni hii inatarajiwa kuadhimishwa duniani kote Mei 16, 2026 ikilenga kuhamasisha jamii kushiriki zaidi katika malezi na maendeleo ya watoto wa kiume.

Waandaaji wa kampeni hiyo wamesema lengo ni kuongeza mjadala kuhusu changamoto zinazowakabili watoto wa kiume, ikiwemo malezi hafifu, ukosefu wa mwongozo na mazingira hatarishi nchini.

Mwanzilishi wa Boys Initiative Tanzania amesema mtoto wa kiume anahitaji malezi bora ili akue akiwa na maadili, uwajibikaji na mchango chanya kwa jamii.

“Tunataka kuona watoto wetu wakipewa nafasi, mwongozo na malezi bora ili wawe sehemu ya maendeleo ya taifa,” amesema.


Kwa upande wake, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imehimiza ushirikiano wa wazazi, walimu, viongozi wa dini na jamii katika malezi ya watoto wa kiume.

Kupitia kampeni hiyo, Boys Initiative Tanzania imesema inaendelea kufanya mijadala ya kijamii, programu za malezi na kampeni za elimu katika maeneo mbalimbali nchini kwa mwaka mzima.

Siku ya Mtoto wa Kiume Duniani huadhimishwa katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuzungumzia ustawi, afya ya akili, elimu na maendeleo ya watoto wa kiume.