Na Mwandishi wetu
Katika kipindi ambacho vijana wengi wanatafuta ajira na njia za kujitegemea, Chuo cha Ufundi Peramiho mkoani Ruvuma kinaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwajengea Watanzania ujuzi wa kazi za mikono.
Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1928 na wamisionari kutoka Ujerumani, sasa kina miaka 98. Kwa muda wote huo, kimeendelea kutoa mafunzo ya ufundi kwa maelfu ya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kupitia Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi kwa njia ya Uanagenzi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, vijana 125 wamepata nafasi ya kusoma chuoni hapo kwa gharama za Serikali.
Mkuu wa Chuo hicho, Frt. Martin Mrope, amesema kati ya vijana hao, 118 wanaendelea na masomo kwenye fani mbalimbali ikiwemo ushonaji, ufundi bomba, useremala, ufundi magari na umeme wa majumbani.
Amesema mafunzo hayo yanachukua miezi minane pekee, ambapo miezi sita ni darasani na miezi miwili ni mafunzo ya vitendo kwenye maeneo ya kazi.
“Lengo letu ni kumpa kijana ujuzi wa kujitegemea na uwezo wa kuanzisha shughuli zake mwenyewe,” amesema Frt. Mrope.
Baadhi ya wanagenzi wanasema tayari wameanza kuona mabadiliko makubwa kupitia mafunzo hayo.
Januari Mwakilambo mwenye umri wa miaka 19 anayesomea ufundi bomba amesema sasa ana uwezo wa kufanya kazi ndogo ndogo za mfumo wa maji majumbani.
Kwa upande wake, Shakira Sinakara amesema alichagua ufundi bomba kwa sababu wanawake bado ni wachache kwenye taaluma hiyo.
“Niliona ni nafasi nzuri kujifunza kazi ambayo inaweza kunisaidia kujitegemea,” amesema.
Mwanagenzi mwingine, Ali Hamis Kaukuya anayesomea umeme wa majumbani, amesema mbali na ujuzi wa kazi, mafunzo hayo pia yanawajengea nidhamu na maadili ya kazi.
“Tumefundishwa kuwa waaminifu kwa wateja na kutunza siri za kazi,” amesema.
Wakufunzi wa chuo hicho wanasema programu ya uanagenzi imekuwa msaada mkubwa kwa vijana wengi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia masomo ya ufundi.
Mkufunzi wa umeme wa majumbani, Dastan Komba, amesema vijana wengi sasa wanapata nafasi ya kujifunza ujuzi ambao unaweza kuwasaidia maisha yote.
Naye Sista Deogratia Mauki amesema wasichana wanapaswa kujitokeza zaidi kwenye fani za ufundi ambazo kwa muda mrefu zimeonekana kuwa za wanaume.
“Ufundi unaweza kumsaidia mwanamke kujitegemea popote alipo,” amesema.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, jumla ya vijana 5,746 wananufaika na programu hiyo katika vyuo 46 nchini.
Serikali imesema mafunzo hayo yanalenga kuwapa vijana ujuzi wa haraka utakao wawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema Serikali pia imetenga Tshs bilioni 1 katika bajeti ya mwaka 2026/27 kusaidia wahitimu kupata vifaa vya kuanzia kazi.
Wadau wa elimu ya ufundi wanasema programu hiyo inaweza kuwa suluhisho muhimu la changamoto ya ajira kwa vijana wengi nchini.
Kwa sasa, simulizi ya Peramiho inaendelea kuonyesha kuwa ujuzi bado ni moja ya silaha muhimu kwa maisha ya vijana wa Tanzania.

